Dk. Magufuli asema atashirikiana na vyama vyote vya siasa kwenye kuiongoza nchi

Posted by Unknown on 21:41 with No comments

Dk. John Magufuli.
Mgombea  urais wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk. John  Magufuli pamoja na mgombea mwenza, Samia Suluhu Hassan, jana waliwasili katika viwanja vya ndege vya Abeid Karume Zanzibar na kupokelewa na umati mkubwa wa wananchi na wanachama wa chama hicho.
 
Katika mapokezi hayo,  Magufuli alisindikizwa kwa msafara wa pikipiki na magari huku wafuasi wa chama hicho wakiwa wamevaa sare zenye rangi ya njano na kijani.
 
Wanachama hao walikuwa na mabango yaliyokuwa na ujumbe unaosema kuwa “karibu Dk. Magufuli rais wa Tanzania wa mwaka 2015/ 2020 bado kuapishwa tu”.
 
Mgombea huyo aliondoka viwanja hivyo na msafara huo ukiwa na ulinzi mkali wa Jeshi la Polisi na maofisa wa Idara ya Usalama wa Taifa ukisindikizwa na wanachama hao na kuelekea katika makao makuu ya CCM Kisiwandui na kuzuru kaburi la Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Hayati  Abeid Amani Karume kisha kuzungumza na wanachama.
 
Dk. Magufuli alisema endapo atachaguliwa kuwa Rais wa, atashirikiana na vyama vingine vya siasa kwa lengo la kuharakisha maendeleo ya Watanzania.
 
“Umoja wetu ambao umeasisiswa na  viongozi wa Chama cha  Mapinduzi tangu enzi za Uhuru ni lazima Watanzania na wana-CCM waendelee kuulinda kwa nguvu zote,” alisema  Dk. Magufuli. 
 
Alisema atahakikisha anasimamia vyema ilani ya uchaguzi ya CCM ili kuleta maendeleo katika sekta mbalimbali za kiuchumi na kimaendeleo ambayo ndiyo nguzo kuu ya kuwakomboa Watanzania.
 
“Ilani ya Chama cha Mapinduzi imezungumzia mambo kibao, tutahakikisha sisi wote wagombea watatu wa CCM na viongozi wengine wa chama tunashikamana kwa pamoja katika kuitetea Ilani ya  uchaguzi ya CCM,” alisema.
 
Alisema endapo atapata ridhaa ya Watanzania na kushinda atahakikisha anashirikiana na Rais wa Zanzibar,  Dk. Ali Mohammed Shein (pichani), kwani kiongozi huyo ni muadilifu na asiyekuwa na majivuno. “Dk. Shein hana majivuno, hana makuu, anampenda Mungu na anawapenda Wazanzibari na Watanzania wote, napenda kuwaahidi wote na hata wasio wana- CCM kwamba nitatoa ushirikiano kwa Dk. Shein ili kuleta maendeleo,” alisema Dk. Magufuli.
 
Naye  Mgombea mwenza kwa tiketi ya CCM, Samia  Suluhu Hassan, alisema uteuzi huo umedhihirisha wazi kuwa chama hicho kimeweka historia kwa kumteua mwanamke katika ngazi ya juu ya uongozi.
Categories: