Madiwani 20 kwa Lowassa wahamia rasmi Chadema.
Posted by Unknown on 12:19 with No comments
Madiwani 20 na wenyeviti sita wa vijiji waliokuwa wakimuunga mkono Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, katika kinyang'anyiro cha kuwa mgombea urais kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), jana wamejiunga rasmi na Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema). Mbali na madiwani hao, wafuasi wa waziri mkuu huyo wa zamani wanaojiita 4U Movement, Team Lowassa na kundi la vijana zaidi ya 200, wa jijini Dar es Salaam, wamesema katika uchaguzi mkuu ujao kura zao wanawapa wagombea wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Huko Monduli, akizungumza katika mkutano wa hadhara, muda mfupi kabla ya kukabidhi kadi za madiwani wenzake 19, kiongozi wa madiwani hao, Julius Kalanga wa kata ya Lepurko, alisema kuwa wamefanya uamuzi huo mgumu baada ya kugundua CCM kinakiuka katiba ya chama hicho kwa kufuata matakwa ya familia za viongozi wachache.
Kalanga alisema kuwa CCM ya sasa imekosa maadili, pamoja na kujisifu kuwa kina maadili. Alisema kinaminya uhuru wa wanachama wake kufikiri chochote nje ya familia ya viongozi wachache wenye kuamua matakwa yao.
Aliwasihi wananchi wote hususan Wamasai jamii ya wafugaji kuwafuata madiwani wao wanakokwenda kwa sababu kama madaraka hata huko watachukua fomu na kugombea ili kuing’oa CCM.
“Lakini tunamuomba sana mheshimiwa wetu Lowassa atufuate huku Chadema afanye maamuzi magumu aliyokuwa akisema kila siku na asiogope akihama atakuwa amefanya uamuzi wenye tija kwa taifa," alisema.
Alisema kwa sasa wanaanza ziara rasmi maeneo yote ya Umasaini kuing’oa CCM kwa sababu ni chama batili kinachokwenda kinyume na katiba yake.
Baada ya kuzungumza na hadhara hiyo alimkabidhi Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Arusha, Amani Golugwa kadi 34 za viongozi wa Wilaya ya Monduli.
Madiwani waliohama chama ni wa kata ya Engaruka, Engutoto, Esilalei, Loksale, Majengo, Makuyuni, Meserani, Nalalani, Lemooti, Moita, Monduli Juu.
Monduli Mjini, Mferejini, Mswakini, Mto wa mbu, Migungani, Selela, Sepeko na Lashaini. Waliohama chama hicho Madiwani na Viongozi mbalimbali ni, Julius Kalanga, Edward Lenanu, Bazir Siamini, Sigur Olekibinti, Loti Yamat, Goodluck Lerunya, Pashet Sengurumi, Yase Runja, Gideon Kimongishu, Dora Kipuyo, Mary Morindat, Sara Lomayan, Halima Lusinde, Dotto Mlacha, hawa Nyambiry, Alex kamanda, Sion Kapela, Maria Lemta, Onesmo Naikoyo, Shaban Adam, Enditosidai Naikulo na Elifuraha Simon.
Wengine ni Dinna Solomon, Loti Naparana, Joyce Laizer, Edward Mathayo, Piniel Loning’o, Napir Mukare, Inot Leringa, Kalaine Lowassa, Maria Mepukori, Mary Stivin na Edward Kone.
Akizungumza baada ya kuwakabidhi kadi, Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Arusha, Amani Golugwa, aliwakaribisha na kusema Chadema watu wote wanapendana na hakuna ukubwa wala uongozi, hivyo wanapokuja huko ni kazi moja ya ukamanda kuwatumikia wananchi.
“Lakini kikubwa tunatubu, tunasameheana, sababu sisi sio malaika wala hatupo imara ni binadamu na hata kama kuna dhambi imefanyika hakuna dhambi nyekundu isiyoweza kusafishwa na kuwa nyeupe kama theluji,”alisema.
Naye Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless lema, alisema Wamasai na wote waliokuwa katika safari ya Matumaini hawana haja ya kukata tamaa, kwani sasa wameanza safari ya ushindi Oktoba, kinachotakiwa kuunganisha nguvu kuing’oa CCM.
Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari alisema Julai 10 mwaka huu, akiwa Dodoma aliwasikia baadhi ya wanaCCM wakisema nchi ya Tanzania haiwezi kukabidhiwa mikononi mwa Wamasai sababu wao ni wachunga ng’ombe tu.
Katika hatua nyingine, Katibu wa CCM Wilaya ya Monduli, Elisante Kimaro, amedai kuwa baadhi ya madiwani wa zamani wameenda ofisini kwake kumuomba radhi kwa kile alichodai wamekihama chama hicho.
Alidai hali hiyo inaonyesha jinsi madiwani hao walivyoanza kusalitiana wenyewe kwa wenyewe.
Alisema madiwani hao ambao anawaita ni makada baada ya Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Monduli kuvunjwa, walifanya mkutano kwa kushawishiwa na mmoja wao.
Alisema ushawishi huo unatokana na uchu wa madaraka alionao kwa kuwa tayari wananchi wa Jimbo la Monduli, wanampenda aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalum CCM, Namelok Sokoine, kuchukua fomu za ubunge wa jimbo hilo.
WATANGAZA KUINGA UKAWA
Makundi matatu yaliyokuwa yanamuunga Lowassa, katika kinyang’anyiro cha kugombea urais wametangaza rasmi kuipigia kura Ukawa kwa kuwa CCM imekataa mabadiliko ikiwamo kutatua kero za wananchi.
Wamesema zaidi ya kura milioni 10 watazitoa kwa mgombea urais wa Ukawa kwa lengo la kupata mabadiliko nje ya chama na sio CCM kwani imeonyesha wameshindwa kutatua changamoto mbalimbali zinazolikabili taifa.
Akizungumza katika mkutano huo kwa niaba ya wafuasi hao, Mratibu Taifa 4U Movement na kiongozi wa makundi ya Vijana wanaomuunga Lowassa, Hemed Ally, alisema kuwa imewalazimu kuhamishia kura zao za urais kwa Ukawa ili waweze kupata mabadiliko ambayo CCM haikubali kwani wao walikuwa na imani na Lowassa.
Alisema kuwa haki haikutendeka sio tu kwa Lowassa bali kwa wanachama wote waliokosa nafasi hiyo na waliopata nafasi hiyo hapakutendeka haki.
Ally alisema wakati umefika bila kukosea kuyasaka mabadiliko nje ya Chama Cha Mapinduzi hivyo wameamua kutangaza rasmi kuwa hawatakiunga mkono CCM.
“Hii haina maana kuwa tuna ugomvi na mgombea urais Dk. John Magufuli, ila katika upatikanaji wake ni kinyume cha utaratibu na haki hivyo tunaiungua mkono rasmi Ukawa,” alisema.
Aliongezea kuwa " Sio kwamba Dk. Magufuli atashindwa kutatua kero tatizo lililopo ni kwamba mfumo uliompitisha hautamruhusu kufanya mabadiliko."
Alishauri Ukawa waunganishe vyama vyote vya upinzani kwani rekodi iliyojionyesha mwaka 2010 Rais Jakaya Kikwete alipata kura milioni 5 sawa na asilimia 61.
“Na sisi 4U Movement tupo milioni 5, timu Lowassa milioni 3.5 na makundi mengine ambayo yanamuunga Lowassa yanafikia milioni 2 hivyo tuna kura zaidi ya milioni 10 ambazo tutawapa Ukawa,” alisema.
Alisema kuwa wameanza rasmi safari ya mabadiliko kuking’oa Chama Cha Mapinduzi katika dola wamechoka na maovu wanayoyafanya na wanayaridhia.
Ally alisema Kingunge Ngombale-Mwiru, alizungumza na wao ni zamu yao kusema safari ya mabadiliko nje ya CCM imeanza rasmi.
Kadi ya chama ni haki ya raia mwenyewe umoja wao upo katika shahada ya kupiga kura na kwamba wapo ambao watabakia Chama Cha Mapinduzi lakini hawatapigia kura CCM.
Kwa upande wake, Kaimu Katibu Mkuu Kinondoni Chadema, Rose Mushi, alisema yeye alialikwa kwa ajili ya kuungana kwa pamoja na wao wapo tayari kuwapokea kwa ajili ya kufanya mabadiliko.
“Mimi nipo hapa leo sio kwamba ni timu Lowassa nimeitwa na mmoja wa viongozi wa makundi hayo kwa madai kuwa wanatoa tamko lao nimekuja kuwasikiliza,” alisema.
Moshi alisema tayari wameshawapokea vijana kutoka katika kundi hilo la Lowassa na ninakiri ni kweli wamechoshwa na siasa wa vyama vingine na ndio maana wameamua kujiunga na Chadema.
WABUNGE WENGINE KUFUATA
Wakati muda wa kuchukua fomu za kugombea ubunge na udiwani ukimalizika leo, baadhi ya wabunge hawajachukua fomu, jambo linaloashiria kuhamia upande mwingine wa vyama vya siasa.
Inasadikika kuwa wapo baadhi ya wabunge katika kanda ya Ziwa, wakiwemo wa viti maalum ambao watavihama vyama vyao na kujiunga na Ukawa muda siyo mrefu.
Categories: NEWS

Wamo pia wenyeviti wa vijiji sita 4U 200 Dar nao wajiunga Chadema, Wabunge wengine wakiwamo viti maalum kufuata.
0 comments:
Post a Comment