Urais CCM saa 120 za presha.

Posted by Unknown on 18:18 with No comments


Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana.
Chama Cha Mapinduzi (CCM), leo kinaanza rasmi vikao vyake vya juu vitakavyotoa jina la mgombea wa urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania baada ya saa 120 zijazo.
 
Vikao hivyo vitaanza leo hadi Jumamosi zikiwa ni siku tano sawa na saa 120 na kutangaza jina la mgombea wa nafasi hiyo siku inayofuata ya Jumapili.
 
Vikao hivyo vitaanza kwa Sekretarieti ya Kamati Kuu ya Taifa (CC) kujichimbia kwa ajili ya kufanya maandalizi ya mfululizo wa vikao vingine, ambavyo vitafanya uamuzi makubwa na magumu ya kuteua mgombea wake wa urais.
 
Vyanzo vya uhakika vimeeleza kuwa, kikao hicho kitakachokuwa chini ya Mwenyekiti wake, Abdurahman Kinana, Katibu Mkuu wa CCM  ni mahususi kwa ajili ya kupanga maandalizi ikiwamo kuweka sawa, taratibu za malazi, chakula, magari na masuala mengine ya kiitifaki kwa wageni walioalikwa.
 
“Hiyo Sekretarieti inakaa kesho (leo) chini ya Kinana kwa ajili ya maandalizi, unajua kuna mabalozi wa mbalimbali, makada wa chama, wajumbe na watu wengine mashuhuri wamealikwa kuhudhuria. Sasa kuna suala la kupanga magari, malazi, watakula wapi na mambo mengine,” kilisema chanzo hicho.
 
NIPASHE ilishuhudia jana wajumbe wa kikao hicho cha Sekretarieti, akiwamo Kinana, Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye wakiwa tayari wamewasili mjini hapa.
 
Taarifa zaidi zinaeleza kwamba wajumbe halali wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), waliothibitika kwamba, ndio watakaoyapigia kura majina matano ya wagombea wa kiti cha urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni 396, huku wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa watakaolipigia kura jina moja kati ya matatu yatakayopelekwa kwao ni 2,400.
 
Mgombea huyo atatoka miongoni mwa makada 38 waliojitokeza na kukamilisha mchakato wa kuchukua na kurejesha fomu za uteuzi wa kumpata atakayepeperusha bendera ya CCM katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu, dhidi ya wagombea wa vyama vya upinzani.
 
Kikao cha Kamati ya Usalama na Maadili kitafanyika kesho.  Vikao vingine ni CC ambayo itakutana Alhamisi na kufuatiwa na kikao cha Nec Ijumaa na baadaye kuhitimishwa na Mkutano Mkuu utakaofanyika Jumamosi na Jumapili.
 
WALIO KATIKA PRESHA
Wagombea waliorejesha fomu na kutarajiwa kuwa katika presha kutaka kujua kama majina yao yatapita kwenye mchujo utakaofanywa wiki hii na vikao vya juu vya maamuzi CCM na mwishowe kupata jina moja la mgombea wa urais ni wagombea wote 38 waliorudisha fomu kufikia saa 10:00 jioni ya Julai 2, 2015.
 
Wagombea hao ni pamoja na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalum), Profesa Mark Mwandosya, Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Steven Wasira, Balozi wa Kudumu wa Umoja wa Afrika (AU), nchini Marekani, Balozi Amina Salum Ali na mtoto wa tano wa hayati Baba wa Taifa, Makongoro Nyerere.
 
Wengine ni Makamu wa Rais, Dk. Mohamed Gharib Bilal, Waziri Mkuu Mstaafu, Federick Sumaye, Amos Siyantemi, Mkurugenzi wa zamani wa Idara ya Usalama wa Taifa (TIS), Dk. Hassy Kitine, Balozi Alli Karume, Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa na Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli.
 
Wamo pia Waziri wa Nishati na Madini aliyejiuzulu, Profesa Sospeter Muhongo, Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta, Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk. Titus Kamani, Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, Naibu Waziri wa Fedha wa zamani na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Monica Mbega, Balozi katika Umoja wa Mataifa, Dk. Augustino Mahiga, Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Januari Makamba na aliyewahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja. 
 
Wengine ni Joseph Chaggama Mbunge wa Nzega, Dk. Hamis Kigwangala, Mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina, Dk. Muzzamil Kalokola, Idelphonce Bilohe, Boniface Ndengo, Waziri wa Sheria na Katiba, Dk. Asha Rose Migiro na Waziri wa Ushirikiano wa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki, Dk. Harrison Mwakyembe.
 
POLISI YAONYA
Wakati hayo yakiendelea, Polisi mkoani Dodoma imeonya kuhusu vitendo vya uvunjifu wa amani kwa makundi ya wapambe wa watangaza nia ya urais ikisema, haitowavumilia watakaobainika kuzusha ama kuandaa vitendo vya kihalifu wakati wa mchakato huo.
 
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, David Misime, alisema ulinzi umeimarishwa ikiwa ni pamoja na doria za miguu, magari, pikipiki, mbwa na farasi.
 
Alisema kutokana na unyeti huo wageni zaidi ya 10,000 wanaotarajiwa kufurika mjini Dodoma ni lazima jeshi hilo liimarishe ulinzi kwa pande zote ili mji uwe salama.
 
“Ili Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya dola waweze kufanya kazi kwa ufanisi, linaomba ushirikiano wa wananchi wa Dodoma na wageni kwa kutupa taarifa pale watakapoona mtu au watu jambo lolote linaloashiria uhalifu ili hatua ziweze kuchukuliwa,” alisema Misime.
 
Aliwaonya wamiliki na wahudumu wa nyumba za kulala kutoshiriki kuhatarisha amani kwa kupokea wageni wasiotaka kujitambulisha na badala yake akawataka kutoa taarifa wanapoona watu au wageni wanaowahisi ni wahalifu.
 
“Wote wanaotaka kuja Dodoma katika wiki hii ya heka heka za CCM, kama hawana shughuli maalum na wanaotaka kuja kwa ajili ya kushuhudia au kushabikia wagombea wa kiti cha urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia CCM, ni vyema wasije ili kuepuka usumbufu utakaojitokeza,” alisema Misime.
 
BARABARA YA BUNGE YAFUNGWA
Katika hali isiyo ya kawaida; vikosi vya usalama vimeifunga rasmi barabara kuu ya Dar es Salaam-Dodoma ambayo hukatisha karibu na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa madai ya kuimarisha ulinzi wa mji wa Dodoma na viunga vyake.
 
Vikosi vya usalama pia vimeweka utepe wa njano, katika  barabara inayoanzia Chuo cha Biashara cha Dodoma (CBE), vikiashiria kwamba barabara hiyo haitumiki huku pia vikiruhusu kutumika kwa barabara ya Mwanza-Dodoma kama barabara mbadala.
 
Kamanda Misime alipoulizwa na NIPASHE sababu za kufungwa kwa barabara hiyo wakati huu ambao mji wa Dodoma unakabiliwa na shughuli nyingi za uchaguzi ndani ya CCM; alisema: 
 
“Barabara ya Bunge, imefungwa kama moja ya hatua za kiusalama za kuimarisha ulinzi kutokana na vikao mbalimbali vitakavyofanyika.”
 
“Hatua hii ya kufunga barabara kuu tunaweza kuieleza kwamba ni trela au bashirafu kwa kuwa ndio namna ya kuimarisha ulinzi wenyewe. 
 
Tutegemee kuona mengi zaidi katika kuhakikisha shughuli zote ambazo zimepangwa kufanyika Dodoma kwa wiki hii, zinaenda kama zilivyopangwa kwa amani na utulivu,” aliongeza.
 
Akizungumzia kuhusu kufungwa kwa barabara hiyo kama kuna uhusiano wa kudhibiti wapinzani bungeni, Misime alisema: 
 
“Hakuna uhusiano wowote wa kufunga barabara kwa sababu ya kuhofia wabunge wa vyama vya upinzani waliopewa adhabu ya kutoshiriki vikao vya Bunge hadi litakapovunjwa na Rais Jakaya Kikwete Julai 9, mwaka huu. Wabunge hao, wameondoka na mimi sina shughuli nao. Hizi hekaheka nyingi ndio jukumu langu.”
 
NIPASHE ilishuhudia pia barabara kuu ya Dar-Dodoma, ikiwa imefungwa kuanzia maeneo ya Ihumwa, kilomita 13 kutoka katikati ya mji, huku ikiwa haina ulinzi wa askari wa Kikosi cha Usalama wa Barabarani.
 
MGOMBEA URAIS AREJESHA FOMU
Wakati huo huo, mtangaza nia wa kiti cha urais, Peter Nyalali ambaye ni miongoni mwa makada wanne waliotajwa kupoteza sifa kutokana na kushindwa kurejesha fomu ya kuomba kuteuliwa na chama hicho kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, amefanikiwa kurejesha fomu hiyo siku tatu baada ya CCM kufunga rasmi mchakato huo. 
 
Nyalali alikabidhi  fomu hizo juzi saa 10:05 jioni, baada ya kujieleza kwamba alichelewa kurejesha fomu yake, akidai kwamba alipewa muda wa nyongeza na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara, Rajab Luhwavi, na kurejesha fomu zake za wadhamini aliotakiwa kuwapata katika mikoa 15 ya kikanuni ikiwamo mitatu ya lazima kutoka Zanzibar.
 
Nyalali ambaye ni miongoni mwa wanasiasa vijana, waliojitosa kuwania kiti hicho, alisema kuwa anaamini kuwa Tanzania, ina tunu ya viongozi shupavu wanaoweza kutetea haki na kuleta usawa kwa wananchi wa Tanzania.
Categories: