WANANCHI WACHOMA MOTO KITUO CHA POLISI CHA BUNJU A
Posted by Unknown on 07:54 with No comments
KITUO cha Polisi cha Bunju A, kilicho Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam, kimechomwa moto na wananchi waliokuwa wakiwatuhumu Askari Polisi kutotekeleza majukumu yao ya kazi kwa ufasaha.
Tukio la kuchomwa kwa kituo hicho limethibitishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, Camillus Wambura, ambaye alisema wachomaji walitekeleza uhalifu huo najira ya saa 3.00 asubuhi.
Akizungumzia tukio hilo lilivyotokea kupitia simu yake kiganjani, Kamanda Wambura alisema kabla ya kuchomwa, gari aina ya Coster iliyokuwa ikiendeshwa na dreva aliyetambulika kwa jina la Yohana John, ilimgonga mwanafunzi wa Shule ya Msingi, Bunju A, aliyetambuliwa kwa jina la Radhia Omary, ambaye alifariki papo hapo.
Kamanda Wambura alisema baada ya tukio hilo la ajali maofisa wa Wakala wa Barabara (Tanroads) na Askari Polisi walikutana kujadili namna ya kuweka matuta eneo hilo baada ya wakazi na wanafunzi wa shule hiyo kulala barabarani kuzuai magari yasipite.
“Wananchi na wanafunzi walifunga barabara hiyo kwa muda saa tatu wakidai kuwa wanataka matuta yawekwe katika eneo lililo karibu na shule ili kuwasaidia wanafunzi wakati wa kuvuka barabara.
“Hali hiyo ilileta usumbufu kwa watumiaji wa barabara. Polisi na Tanroads tulikaa kikao cha dharura kuangalia namna ya kuweka matuta haraka lakini wakati tukiendelea kujadili wananchi walipata mwanya, wakivamia kituo wakakichoma moto.
“Mbali na kuchoma kituo, pia walichoma magari manne ya watu binafsi yaliyokuwa yameegeshwa pembezoni mwa kituo,” alisema Kamanda Wambura.
Alisema Polisi wanamshikilia dreva wa Coaster aliyesababisha ajali pamoja na watu wengine watano na wanaendelea kuwasaka wengine waliosababisha kutokea kwa vurugu.

Moshi mkubwa kutoka eneo hilo la kituo.

Categories: NEWS

0 comments:
Post a Comment