Ukawa wadai safari za JK zimekula Sh4 trilioni
Posted by Unknown on 10:12 with No comments


Rais Jakaya Kikwete
Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) umedai Rais Jakaya Kikwete amefanya safari 409 nje ya nchi katika kipindi cha utawala wake, akitumia zaidi ya Sh4 trilioni, fedha ambazo zingeweza kutumika kwa miradi ya maendeleo.
Ukawa pia imemtaka mwenyekiti huyo wa CCM kuwa tayari kujitokeza kwenye midahalo dhidi ya wenyeviti wa umoja huo ili kufafanua ilani za vyama vyao kwa wananchi.
Mwenyekiti mwenza wa Ukawa, James Mbatia alitoa madai hayo juzi usiku alipozungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari uliorushwa moja kwa moja na vituo vya televisheni. Mbatia aliandaa mkutano huo kwa ajili ya kuzungumzia mambo mbalimbali kuhusu maendeleo ya mchakato wa Uchaguzi Mkuu.
Mbatia alisema katika kipindi hicho, Rais Kikwete alifanya safari ambazo baadhi hazina umuhimu, akitoa mfano wa safari za kupokea digrii za heshima, kazi ambayo alisema ingeweza kufanywa na mabalozi.
Alisema Sh4 trilioni zingeweza kutumika kwenye ujenzi wa vyuo vya ufundi, vyuo vikuu au hospitali kama safari za Rais zingepunguzwa.
Lakini Mbatia alisema tangu mwaka 2005 wakati Kikwete alipoingia Ikulu kwa mara ya kwanza ni chuo kimoja tu cha Veta kimejengwa mjini Makete.
“Ukawa tukiingia ikulu, tutapunguza safari za rais kwa asilimi 80. Matukio ya kwenda kupokea digrii za heshima yatahudhuriwa na mabalozi waliopo huko,” alisema Mbatia.
Akiweka msisitizo kwenye hoja hiyo, mshauri wa Chadema, Profesa Mwesiga Baregu alisema kwa kipindi chote cha miaka kumi, Rais amekuwa wa nje ya nchi na mara kadhaa amekuwa akitoka kwenda kuomba misaada wakati Taifa linaweza kujitegemea.
“Rais akiwaingilia sana mabalozi kwenye maeneo yao ya kazi, hataweza kuwawajibisha. Safari zake za nje pia zinaongeza gharama za kutokuwepo nyumbani pamoja na ile ya aliowapa dhamana,” alisema.
Mdahalo
Katika mkutano wake wa juzi, Mbatia pia alizungumzia muhimu wa midahalo, akisema inafaa kwa ajili ya kuelimisha Watanzania kitakachofanywa na vyama hivyo endapo kimoja kati yao kitashinda Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25.
Alimtaka Kikwete kujitokeza hadharani na kuitetea ilani ya CCM kwenye mijadala ya pamoja na yeyote kati ya wenyeviti wa vyama vinavyounda umoja huo, ambavyo ni Chadema, NLD, CUF na NCCR Mageuzi.
“Tunakaribisha midahalo na chama tawala ili tuziuze ilani zetu kwa Watanzania. Atoke mwenyekiti wa CCM na akabiliane na (mwenyekiti wa Chadema, Freeman) Mbowe, (mwenyekiti wa NLD, Dk Emmanuel) Makaidi au mimi mwenyewe. Sisi tumetoa ilani ya pamoja ambayo mgombea wetu anaitumia hivyo yeyote anaweza kuisemea,” alisema Mbatia.
Alisema kwenye chaguzi zote zilizopita, ahadi nyingi zilitolewa lakini wananchi hawakupata wasaa wa kujua ni namna gani ilani hizo zitatekelezwa.
Makamba amjibu Mbatia
Lakini msemaji wa CCM kwenye shughuli za kampeni, January Makamba alimshangaa Mbatia kwa kutaka midahalo ihusishe wenyeviti wa vyama badala ya wagombea, akisema hakuna kitu kama hicho duniani.
Makamba alisema wiki tatu zilizopita, CCM ilipata mwaliko kutoka Baraza la Habari Tanzania (MCT) ikimtaka Magufuli kushiriki katika mdahalo huo na Dk Magufuli amekubali kushiriki.
“Kauli iliyotolewa na Mbatia kwamba Ukawa inaomba mdahalo, ni kuwahadaa Watanzania kwa kuwa mwaliko ulishatolewa mapema kwa vyama vyote vya siasa,” alisema na kuongeza kuwa midahalo hiyo iwe ni ya wagombea.
“Hoja hii ni ya kichekesho kwani midahalo haifanywi na wenyeviti kwa niaba ya wagombea. Wagombea ndiyo wanaopaswa kujibu maswali na kufafanua ahadi zao,” alisema.
Matokeo ya uchaguzi
Mbatia pia alisema kuwa Watanzania wana kiu ya mabadiliko na Ukawa imejizatiti kufanya mabadiliko na ina watu wenye uzoefu wa kuyaongoza, hivyo CCM isifanye njama za kuhujumu matokeo.
“Wanachokitaka Watanzania kipo Ukawa na ni wao ndiyo watakaopiga kura na kuupa ushindi umoja huu hivyo CCM iwe makini na ujanja wowote inaotaka kuufanya,” alisema Mbatia.
“Endapo CCM watatumia hila kutupora ushindi wetu utakaotokana na kura za wananchi, nawahakikishia Watanzania wataidai haki yao kwa ajili ya nchi yao. Kwa mapenzi ya dhati watampigania Mama Tanzania,” alisema.
Lakini Makamba aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa Ukawa ndio wanaoandaa watu kufanya vurugu kutokana na kauli zao za kudai kuwa CCM itaiba kura.
Alisema kauli hizo zinaashiria maandalizi ya kushindwa na wanafanya hivyo ili kuwatayarisha wananchi waamini kwamba kuna wizi wa kura ili wafanye vurugu.
Alisema utaratibu uliokubaliwa na vyama vyote vya siasa ni kuwa kura zinapigwa kituoni mbele ya mawakala wa vyama vyote.
Alisema baada ya kura kupigwa zinahesabiwa na matokeo yanajazwa katika fomu ambayo kila wakala anasaini na kupewa nakala.
“Matokeo ya nchi nzima yanajumlishwa mahali pamoja huku kukiwa na waangalizi wa uchaguzi wa ndani na nje ya nchi.” Alisema matokeo hayo ya kura yanajumlishwa mbele ya wawakilishi wa vyama vyote na wao wakiwa na fomu zao za kila kituo nchi nzima.
Azungumzia kauli ya Magufuli
Pia, Mbatia alizungumzia kauli iliyowahi kutolewa na Dk Magufuli kuwaonya wananchi kuchagua wapinzani kuwa inaweza kutumbukia nchi kwenye machafuko kama ilivyokuwa Libya.
Alisema kauli hiyo inalenga kujenga hofu miongoni mwa wananchi kwa kuwaaminisha kitu kisichokuwepo juu ya upinzani na mustakabali wa Taifa lao. “Nimeshangazwa na kauli ya mwenyekiti wa NEC eti kauli kama hiyo ni vionjo vya kisiasa badala ya kuchukua hatua na kukemea,” alisema.
Alisema kuondoka kwa viongozi wao, wakiwamo waliowahi kuwa mawaziri wakuu; Edward Lowassa na Fredrick Sumaye, mawaziri wengine na wenyeviti wa CCM kusionekane ni jambo baya kiasi cha kutoa kauli nyingi za uzushi wa kuwatisha wananchi wanaotaka mabadiliko ya mfumo usiokuwa na tija.
Categories: NEWS
0 comments:
Post a Comment