Kortini kwa kutumia majina ya CCM, Chadema
Posted by Unknown on 13:08 with No comments


Mwanza. Watu watatu wamefikishwa Mahakama ya Mkoa wa Mwanza wakikabiliwa na mashtaka ya wizi wa kimtandao na kujipatia Sh4 milioni kwa njia ya udanganyifu.
Washtakiwa hao wanadaiwa kusajili namba za simu za uongo, huku wakifungua akaunti ya benki ya NMB kwa jina la vyama vya Chadema na CCM wakitaka wachangiwe fedha za kuendesha kampeni za Uchaguzi Mkuu.
Wakili wa Serikali, Castuce Ndamugoba aliwataja washtakiwa hao kuwa ni Bony Tefe (40), mkazi wa Mahina, Spridon Njunwa (38) mkazi wa Igoma, na Briton Wilson (43) ambaye ni fundi cherehani na mkazi wa Bugando, Mwanza.
Akiwasomea mashtaka jana mbele ya Hakimu Mkazi, Abeisiza Kalegeya, Wakili Ndamugoba alidai washtakiwa wanakabiliwa na makosa manne ya kughushi, kula njama, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na wizi kwa njia ya mitandao.
Alidai kuwa kwa pamoja kati ya Oktoba na Novemba mwaka huu, washtakiwa wote kwa pamoja wakiwa mkoani Mwanza walikula njama na kutenda kosa la kughushi.
Wakili Ndamugoba alidai Oktoba 2 washtakiwa wote kwa pamoja walifanya udanganyifu kwa kufungua akaunti benki ya NMB inayoonyesha imefunguliwa na CCM Spridon Dini, jambo ambalo alidai halikuwa kweli.
Kosa la tatu, washtakiwa wanadaiwa kushirikiana kughushi barua iliyoonyesha imetolewa na Halmashauri ya Jiji la Mwanza na kosa la nne ni kujipatia Sh4 milioni kwa njia ya udanganyifu kutoka kwa mtu aliyetambulika kwa jina moja la Omega, wakidai wao ni CCM awasaidie kwa ajili ya kampeni za uchaguzi mkuu halafu baada ya uchaguzi watamfikiria.
Wakili Ndamugoba aliomba mahakama kutowapa dhamana washtakiwa, kwani upelelezi unaoendelea.
Washtakiwa wote walikana mashtaka na kuomba mahakama kuwapa dhamana.
Hakimu Kalegeya alisema makosa hayo yana dhamana na alimtaka kila mshtakiwa awe na wadhamini wawili mmoja kati yao awe na vitambulisho vya kazi kutoka ofisi inayotambuliwa na barua zinazoonyesha makazi yao halisi.
Pia, aliwataka wadhamini kusaini bondi ya Sh2 milioni, lakini washtakiwa wote walishindwa kutimiza masharti na kurudishwa rumande hadi Novemba 30, kesi itakapotajwa tena.
Categories: NEWS
0 comments:
Post a Comment