Watoa huduma za afya watakiwa kuacha kuisingizia NHIF

Posted by Unknown on 07:53 with No comments


Kaimu Mkurugenzi wa NHIF,Michael Mhando
Kaimu Mkurugenzi wa NHIF,Michael Mhando 
By Bakari Kiango, Mwananchi
Dar es Salaam.Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), umewataka watoa huduma za afya, kuwajibika kwa ufanisi na kuacha kutoa visingizio kuwa NHIF, inachelewesha kulipa fedha za wanachama.
Akizungumza na Waandishi wa Habari jana, Kaimu Mkurugenzi wa NHIF,         Michael Mhando alisema, kuwa mfuko una jukumu la kuvilipa vituo vya afya kwa kufuata sheria, kanuni na  taratibu katika ulipaji wa fedha hizo kutokana na huduma  wanazopewa wanachama wake.
Alisema  katika kipindi hiki baadhi ya watoa huduma wamekuwa wakitoa sababu mbalimbali za kushindwa kutoa huduma za afya kwa ufanisi, kwa wanachama wa NHIF na wananchi kwa madai ya kukosa fedha za kununua dawa, vifaa tiba na vitendanishi.
 “Visingizio hivi vinajenga mazingira kuwa NHIF, ni kikwazo katika ufanisi wa vituo vya afya. Jambo hili si la kweli na linabeba taswira ya kuleta chuki  baina ya wanachama, wananchi na chombo ambacho kina dhamana ya kutibiwa na mfuko huu,” alisema Mhando.

Aliongeza kuwa NHIF, imekuwa ikifanya jitihada za kuwalipa watoa huduma , ndani ya muda uliowekwa kisheria na unaonekana katika mikataba ambayo mfuko huo umeingia na watoa huduma hao.
Alifafanua kwamba kisheria, madai yanatakiwa kulipwa ndani ya muda wa siku 60, baada ya kuwasilishwa NHIF.  Muda unaweza ukapungua zaidi kutokana na umakini wa kituo husika wa kuwasilisha madai kwa wakati na kwa usahihi.
“Licha ya jitihada hizi, kuna  changamoto zinazojitokeza kwa ni baadhi ya watoa huduma wa vituo vya Serikali hasa katika ulipaji wa madai yao. Hawa wamechelewashaji wa madai wanaoyotudai,” alisema.
Pia, alisema  mfuko huo, umeandaa mfumo wa kieletroniki ambao hospitali zote kubwa ikiwamo Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH),  ambazo zinalipwa zaidi ya Sh5 milioni, zimeingizwa katika mfumo huo ili kuharakisha malipo yanayodaiwa
Hata hivyo, Mhando alisema ili kukabiliana na changamoto hizo NHIF, umelenga kuwawezesha watoa huduma afya kwa kuwapa mafunzo kwenye maeneo yao ya kazi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Masoko na Utafiti wa NHIF, Rehani Athumani  alisema wataweka mfumo mpya wa kutoa taarifa kuhusu mfuko huo ,ili kuwarahisishia wananchi kupata  taarifa zinazohusu NHIF.
Alisema  wanatarajia kuanza majaribio ya  mfumo huo    katika Hospitali  za  Muhimbili, Mwananyamala na Taasisi ya Tiba na  Mifupa Muhimbili  (MOI).

Categories: