Kero za wakulima wa miwa Mikumi zatafutiwa dawa
Posted by Unknown on 18:05 with No comments

Mbunge wa Mikumi, Joseph Haule maarufu kwa jina la ‘Profesa J’ amewaomba wakulima wa miwa wa bonde la Ruhembe kumpa wiki mbili za kujibu kero za Kiwanda cha Sukari Kilombero baada ya kukutana na viongozi wa kiwanda hicho na wa Serikali.
Haule alitoa ombi hilo wakati akizungumza kwenye mkutano wa viongozi wa vyama vya wakulima na wawakilishi wa kiwanda hicho jana.
Alisema wakati umefika wa kumaliza kero na changamoto wanazozipata wakulima hao ambao wamekata tamaa na kuamua kulima mpunga badala ya miwa.
Haule alisema atakutana na viongozi wa vyama vya wakulima wa miwa, mkuu wa wilaya, mkuu wa mkoa na waziri mkuu kisha kuitisha mkutano wa wakulima na kuwaeleza yaliyojiri.
Meneja Uhusiano wa Kiwanda cha Sukari Kilombero, Henry Muchunguzi alithibisha kuwapo kwa changamoto hizo na kuahidi kuzifikisha kwa uongozi wa juu wa kiwanda hicho.
Alisema wakulima wa miwa ni wadau muhimu kwa uhai wa kiwanda hicho, hivyo lazima changamoto hizo zifanyiwe kazi kwa kushirikiana na Serikali akiwamo mbunge wa jimbo hilo na vyama vya wakulima wa miwa.
Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Mkoa wa Morogoro, Devota Minja alisema wameamua kushughulikia kero za wakulima wa miwa huku akimuomba waziri mkuu kuvigeukia viwanda vya sukari nchini.
Alisema vyama hivyo vimekuwa vikiwanyonya wakulima ambao ndiyo wazalishaji wakubwa.
Minja alisema viwanda vya sukari ni moja ya vyanzo vya mapato ya nchi, lakini Serikali imekuwa ikishindwa kusimamia haki na masilahi ya wakulima.
Mmoja wa wakulima hao, Mohamed Kapyale ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kijiji cha Ruhembe alisema wenyeviti wa vyama vya wakulima wa miwa wamekuwa mawakala wa viongozi wa kiwanda hicho.
“Hakuna mkulima wa miwa katika bonde la Ruhembe anayeweza kuondoa umaskini kama Serikali haitaingilia kati na kusimamia masilahi yake na kwa hatua tuliyofikia tunamuomba Rais John Magufuli aje hapa aone wananchi tuliopanga foleni kutwa nzima kumchagua, leo hii tutanyanyasika,” alisema.
Kapyale alisema zao hilo limekuwa chanzo cha umaskini kwa kuwa gharama za uzalishaji ni kubwa kuliko faida wanayoipata.
Alisema hali hiyo inasababisha wakulima kuingia madeni ya mikopo kwenye taasisi za fedha na wengine kushindwa kupeleka watoto wao shule.
Categories: NEWS

0 comments:
Post a Comment