Majaliwa awapa vigogo kauli ngumu
Posted by Unknown on 11:50 with No comments


Watumishi wa serikali wametakiwa kuhakikisha kila mmoja anatimiza wajibu wake wa kuwahudumia wananchi kikamilifu.
Aidha, wakurugenzi wa halmashauri zote nchini wametakiwa kuhakikisha wanashughulikia ipasavyo kero za wananchi katika maeneo yao na kuacha mazoea ya kukaa ofisini tu na kuonya atakayeshindwa atawajibishwa.
Maagizo hayo yalitolewa na Waziri Mkuu, Kasimu Majaliwa, wakati akizungumza na watumishi wa serikali, mkoani hapa jana.
Alisema kila mtumishi anatakiwa kujituma katika utendaji kazi na kuondoa kero zinazowakabili wananchi ili waweze kuiamini serikali iliyopo madarakani kwa kuwapelekea maendeleo.
Alisema kila mtumishi anatakiwa kuhakikisha anatatua kero za wananchi hasa wa vijijini ili kuwapatia maendeleo.
“Kumbukeni serikali ina sera yake ya kuhakikisha kila mtu anafanya kazi kwa mujibu wa sheria na kanuni za kazi. Kila mmoja akifanya kazi zake kwa uadilifu wananchi wataona serikali yao jinsi inavyofanya kazi ya kuwaletea maendeleo,” alisema.
Majaliwa aliwataka wakurugenzi wa halmashauri kuandaa taratibu za majukumu yao ya kazi na bajeti wanazozipanga zihakikishe zinalenga mahitaji ya wananchi na kuacha tabia ya kukaa maofisini badala yake waende kwa wananchi kushughulikia changamoto zinazowakabili.
Aidha, aliwataka wakurungezi hao kuhakikisha kwamba watumishi wanafika ofisini kwa wakati na watakaokiuka wachukuliwe hatua kali za kinidhamu na kumaliza kero za wananchi katika ardhi ili kuepukana na migogoro katika sekta hiyo.
Waziri Mkuu alisema migogoro mingi inayotokea kati ya wakulima na wafugaji ni kutokana na wakurugenzi kushindwa kusimamia kikamilifu maeneo ya wakulima na wafugaji na kusababisha makundi hayo kupambana na kupoteza maisha ya watu.
Pia alizitaka halmashauri zote kuhakikisha zinatenga maeneo ya wafanyabiashara ili kuondoa migogoro kwa wananchi.
“Ninachotaka ni kuona migogoro ya ardhi inamalizika katika halmashauri zote, atakayeshindwa kutimiza wajibu wake tutamuondoa na kumweka mwingine ambae ataendana na kasi ya serikali ya awamu wa tano,” alisisitiza.
Halkadhalika, Majaliwa alizitaka halmashauri kuhakikisha wanaboresha madawati katika shule za msingi na sekondari ili wanafunzi waweze kusoma wakiwa wamekaa na kuongeza ufaulu katika masomo yao.
Categories: NEWS
0 comments:
Post a Comment