Ada elekezi kufunga shule binafsi

Posted by Unknown on 09:58 with No comments




Wanafunzi wakiwa darasani. Baadhi ya shule za binafsi nchini zinaweza kuwa katika wakati mgumu kutokana na mpango wa Serikali wa kuandaa ada elekezi. 

Dar es Salaam. Uamuzi wa Serikali kuandaa ada elekezi kwa vyuo, shule za msingi na sekondari zinazomilikiwa na watu binafsi au mashirika ya dini, unatarajiwa kuwaweka wamiliki wake katika wakati mgumu na huenda ukawa mwanzo wa mwisho wa baadhi ya shule.
Uchunguzi wa Mwananchi uliofanywa kwa miezi miwili sasa umeonyesha kwamba baadhi ya shule zitaathirika vibaya, ikiwa ada elekezi itakayotangazwa na Serikali itakuwa chini ya viwango vinavyotozwa na shule hizo sasa.
Hadi sasa Serikali bado inachanganua mapendekezo ya ada mpya, huku ikiwataka wazazi wenye watoto kwenye shule binafsi, kulipia ada inayotozwa sasa lakini iwapo ada elekezi itakuwa chini ya kiwango wanacholipa sasa, fedha zilizozidi zitakuwa mali ya wazazi, kwa mujibu wa msemaji wa wizara.
Baadhi ya shule hutoza ada kati ya Sh400,000 na Sh900,000, lakini malipo mengine ya chakula na michango hufanya gharama kufikia zaidi ya Sh3.0 milioni.
Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Shule na Vyuo Binafsi (Tamongsco), Benjamin Nkonya ametetea ada hizo akisema zinatokana na mzigo wa kodi zinazokusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), malipo mengine serikalini na gharama kubwa za uendeshaji.
Nkonya alitaja aina kumi na moja (11) ya kodi na malipo mengine yanayokusanywa kila mwaka kwa shule binafsi kuwa ni: Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT), kodi ya tozo la ujuzi (SDL) kutegemea ukubwa wa shule, tozo kwa ajili ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Tanzania.
Malipo mengine ni kwa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra), Idara ya Uhamiaji, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Wakala wa Afya na Usalama Kazini (Osha).
Pia, shule binafsi hulipa tozo Wizara ya Nchi ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi sasa imehamishiwa Ofisi ya Rais), kodi za majengo, huduma za jiji, na huduma za mabango.
Nkonya anasema endapo Serikali isingetoza kodi hizo, ada za shule binafsi zingeweza kupunguza kwa asilimia 30 kwa kuwa malipo hayo ni wastani wa asilimia 30 ya mapato yanayokusanywa na shule binafsi ambazo ni zaidi ya 1,400 zilizopo.
“Kwa mfano, kama mwanafunzi analipa ada ya Sh2.5 milioni, angeweza kulipa Sh1.7 milioni tu lakini inakuwa vigumu kwa sababu ya mrundikano wa kodi hizo,” anasema.
Mkurugenzi wa huduma na elimu kwa mlipa kodi wa TRA, Richard Kayombo anakubaliana na madai hayo.
“Walichosema ni sahihi, kodi tunachukua, lakini kama wanaona ni tatizo basi walishawishi Bunge ambalo lina nguvu ya kutunga na kuboresha sheria. Sisi tunatekeleza tu hizo sheria,” alisema Kayombo.
Msemaji wa Sumatra, David Mziray alitaja malipo kwa basi dogo aina ya Toyota Hiace kuwa Sh30,000, Toyota Coaster aina ya PAX (Sh4,000), na Toyota Coaster (Sh85,000).
“Ukubwa wa kodi ya leseni kwa biashara kwa mwaka inategemea ukubwa wa basi lenyewe,” anasema Mziray.
Lakini Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Dk Joyce Ndalichako hakubaliani na malalamiko ya kodi ya jengo.
“Wasione kuanzisha shule ni kumkomoa mwanafunzi na wapunguze michango isiyokuwa na tija,” alisema Waziri Ndalichako ambaye aliwahi kuwa katibu mtendaji wa Baraza la Mitihani la Taifa (Necta).
“Kwa nini uombe mchango wa jengo? Hivi mtu alipata usajili bila kuwa na majengo? Ili uwe na shule lazima uwe na jengo. Na huyu aliyemsajili atatueleza alitoaje usajili wakati mtu hana jengo,” alisema Ndalichako.
Ada na matumizi
Mwaka 2012, mtafiti Steve Lee aliyedhaminiwa na Benki ya Dunia alitoa ripoti iliyoonyesha Serikali inatumia dola 1,780 (Sh3.5 milioni) kuhudumia mwanafunzi mmoja kila mwaka.
“Sisi tunatumia Sh2 milioni kwa huduma zote za mwanafunzi mmoja kila mwaka,” alisema Nkonya.
“Serikali inakadiriwa Sh4 milioni kutokana na gharama kubwa ya manunuzi. Sheria ya Manunuzi (PPRA) inachangia gharama sana. Kwa mfano, kalamu moja ya Sh1,000 inaweza kununuliwa kwa Sh10,000.”
Charles Totela, mmiliki wa shule ya msingi na sekondari za Charles Totela zilizoko Mbezi Luis anasema kuna jumla ya wanafunzi 45. Ada ni Sh600,000, na wanafunzi kumi kati ya hao wa shule ya msingi wanalipa Sh1.1 milioni, hivyo makusanyo yote ni Sh32 milioni kwa mwaka.
Totela, aliyewahi kuwa mkuu wa wilaya za Hai (1982-87), Monduli (1987-89), Dodoma Vijijini (1990-92), Sumbawanga (1992-94), Kwimba (1994-95) na Geita (1995-97), anasema matumizi kwa mishahara na gharama nyingine za uendeshaji ni Sh39 milioni, sawa na hasara ya Sh7 milioni.
“Kwa sasa niko kwenye vikao na wazazi vya kuongeza ada ya sekondari kwa kuwa nimepanga kuifunga. Ila nasubiria majibu ya wazazi ambao nusu wamekubali niongeze kutoka Sh600,000 hadi Sh1 milioni,” anasema.
Msafiri Mpendu, ambaye ni mmiliki wa Shule ya Msingi na Sekondari ya Lamoon, iliyopo jengo la Machinga Complex jijini hapa, anasema ana wanafunzi 700 ambao wanalipa ada ya Sh900,000. Mapato ya mwaka ya ada ni Sh630 milioni.
“Natumia Sh84 milioni kwa mishahara ya walimu 45, na wafanyakazi 11 (Sh24 milioni), huduma za afya kila mwanafunzi Sh10,000 (jumla Sh7milioni), maji na umeme (Sh7.2milioni), chakula shule ya msingi (Sh36 milioni), kodi ya jengo la shule (Sh84 milioni), gharama ya vitabu (Sh140 milioni),” anasema.
Gharama nyingine ni ada ya mitihani (Sh20 milioni) kwa kuwa inatumia mtaala wa Uingereza. Hivyo jumla ya matumizi ni Sh.540 milioni kwa mwaka.
“hapo, sijaweka kodi za Serikali ambazo zimekuwa nyingi. Pia, ni asilimia 75 ya wanafunzi wenye uhakika wa kukamilisha ada kwa mwaka, kwa hivyo utaona mtazamo wa biashara unapotea kabisa,” alisema Mpendu.
Mpendu anapendekeza ada elekezi iwe kuanzia Sh3.5milioni na kuendelea kama utafiti wa Benki ya Dunia ulivyobainisha, chinin ya hapo itaathiri shule binafsi.
Sama Ndabile, mwalimu mkuu wa shule awali na msingi ya Sahara iliyopo Mabibo jijini hapa, anasema wana wanafunzi 350. Kwa shule ya kutwa ada ni Sh1.5milioni na bweni ni Sh2.5milioni na hivyo wanaweza kukusanya zaidi ya Sh350 milioni.
“Hapo tuna wafanyakazi 25 ambao wanalipa wastani wa Sh20 milioni kwa mwezi (Sh120 milioni kwa mwaka); sijaweka gharama ya chakula na huduma nyingine za umeme, maji na shughuli za shule,” anasema.
Ndabile anasema walipanga kupandisha ada kwa mwaka ujao, lakini ikashindikana kwa sababu ya zuio la Serikali. “Ada hii iliyopo ilipigiwa hesabu ya kipindi cha mchele kilo moja ukiuzwa Sh1400 lakini sasa ni Sh2200; nyama ilikuwa Sh5000 lakini sasa ni Sh7000. Kwa mazingia hayo lazima utapandisha ada na siyo kupunguza kama serikali inavyotaka kulazimisha,” anasema.
Uchunguzi unaonyesha Shule ya Sekondari ya Kidugala Seminari mkoani Njombe pamoja na michango mingine hutoza zaidi ya Sh2 milioni; Kawawa Sekondari (Iringa) Sh1.6 milioni; St Florence (Mikocheni) Sh2.05 milioni kwa kutwa na Sh2.9 kwa bweni; na Shule ya Sekondari ya Feza Sh5.2 milioni.
Green Acres (Tegeta-Salasala) inatoza Sh400,000 kutwa na Sh550,000 bweni; Sahara (Mabibo) Sh1 milioni kutwa na Sh2.2 milioni bweni.
Afisa tawala wa taasisi ya Eckernforde ya jijini Tanga, David Njau anasema kuna gharama nyingi za uendeshaji wa shule.
“Tumenunua vifaa vya maabara kwa masomo ya sayansi vyenye thamani ya Sh62 milioni. Sasa kama ada itakuwa Sh150,000 kwa shule za kutwa na Sh350,000 kwa bweni, zitarejeshwa vipi?” anahoji.
Afisa tawala huyo anasema shule za sekondari zilizo chini ya taasisi hiyo kwa wanafunzi wa kutwa ada ni Sh 400,000 na bweni Sh 1.5 milioni lakini gharama kubwa ni kwenye chakula cha wanafunzi.
“Gharama ya chakula kwa kila mwanafunzi kwa siku moja ni kati ya Sh2,500 na Sh3,000 kwa chakula aina ya wali, nyama, mchicha na maharage na ni lazima ale hata siku za mapumziko kwa sababu yupo bwenini. Hivyo, kwa mwaka mzima ni fedha nyingi,” anasema Njau.
Mwenyekiti mstaafu wa bodi za shule za sekondari za serikali na binafsi mkoani Tanga, Dk Muzzamil Kalokola anasema Serikali inayojali sekta binafsi haiwezi kuingilia masuala ya ada zinazotozwa kwa sababu inaweza kuziua.
Kauli ya Serikali
Kamishina wa Elimu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Eusella Bhalalusesa alisema utafiti bado unaendelea hivyo wadau wote wanayo nafasi ya kuwasilisha maoni yao.
Profesa Eusella Bhalalusesa amezitaka shule binafsi kutopandisha ada zake na kuzingatia agizo la wizara hiyo hadi itakapokamilisha maandalizi ya ada elekezi.
Profesa Bhalalusesa alisema ada zilizopo kwa sasa zitabakia kama zilivyo na kwamba shule itakayokiuka maagizo ya serikali kwa kupandisha, ada hiyo haitatambuliwa.
“Wataalamu watakapokamilisha ripoti yao kabla ya mwaka wa masomo 2016, tutaichambua na wadau wote kabla ya kuanza majaribio yake, lakini kwa sasa lazima wazingatie maagizo hayo ya mwongozo,” alisema.
Alitaja vigezo vitakavyotumika kupanga ada elekezi kuwa ni huduma zinazotolewa na shule, eneo la shule na mmiliki wake.
“Jambo jingine ni kutenganisha mtoa huduma na mfanyabiashara ili kutoza kodi. Tutaangalia kuona shule inayotoa huduma na inayofanya biashara ili anayekua kwa kiwango cha biashara atozwe kodi,” alisema.
*Imeandikwa na Kelvin Matandiko, Tumaini Msowoya, Burhani Yakub     
 0.2k
Categories: