Wagombea Zanzibar wampinga Jecha.

Posted by Unknown on 12:29 with No comments


Mwenyekiti wa Zec, Jecha Salim Jecha.
Wakili wa Mahakama Kuu Zanzibar, Awadhi Ali Said, amesema hakuna sheria iliyovunjwa na wagombea walioamua kujiondoa katika uchaguzi marudio visiwani humo uliopangwa kufanyika Machi 20, mwaka huu.
 
Amesema wagombea hao hawajavunja sheria kwa kutowasilisha majina ya wadhamini wao Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), pamoja na tamko la kiapo cha mahakama cha kujitoa kama alivyoeleza mwenyekiti wa tume hiyo, Jecha Salim Jecha, kwa alichodai walikula kiapo na kufanyiwa uteuzi na tume kwa ajili ya uchaguzi wa Oktoba 25, mwaka jana na sio uchaguzi huo wa marudio.
 
Akizungumza na Nipashe mjini Zanzibar jana, Awadhi ambaye alikuwa mmoja wa makamishna wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyokuwa ikiongozwa na Jaji Joseph Warioba, alisema wagombea wote katika uchaguzi huo wamepoteza sifa kwa sababu uchaguzi wenyewe unafanyika kinyume cha Katiba na sheria ya uchaguzi ya Zanzibar namba 11 ya Mwaka 1984.
 
Naye Mkurugenzi wa Uchaguzi wa CUF, Omar Ali Shehe, alisema mwenyekiti wa ZEC amewadaganya wananchi wa Zanzibar kuwa wagombea wote ni halali katika uchaguzi wa marudio.
 
Alisema wagombea wa urais, uwakilishi na udiwani walikula kiapo na kufanyika uteuzi wa mwisho Septemba 6, mwaka jana kwa ajili ya kushiriki uchaguzi wa Oktoba 25, mwaka jana na sio uchaguzi wa marudio wa Machi 20, mwaka huu.
 
Jecha juzi alisema kuwa, wagombea wote walioandika barua za kujitoa kwenye uchaguzi huo wa marudio bado tume inawatambua kuwa na wagombea halali wa uchaguzi huo.
 
Alisema kuwa kwa mujibu wa kanuni ya 28 ya sheria ya uchaguzi ya Zanzibar , muda wa mgombea kujitoa ulifikia kikomo Septemba 6, mwaka jana, baada ya tume kukamilisha uteuzi wa wagombea kabla ya kufanyika uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka jana.
 
Wakati huohuo,  Chama cha ACT-Wazalendo kimepinga kauli ya Jecha kuwa kitashiriki marudio ya uchaguzi huo.  
Ofisa Habari wa chama hicho, Abdallah Khamis, alisema hayo jijini Dar es Salaam jana,  alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari.
 
Alisema  chama hicho hakitabadili kauli wala kurudi nyuma katika uamuzi wake ya kutoshiriki, kikiamini kuwa hakuna sababu ya kufanyika uchaguzi mwingine nje ya ule uliofanyika Oktoba 25, mwaka jana.
Categories: