Kodi mpya za serikali.

Posted by Unknown on 21:19 with No comments




WAKATI muswada wa Sheria ya Fedha ya Mwaka 2016 ukitarajiwa kuanza kujadiliwa bungeni leo ambao unaoipa serikali mamlaka ya kisheria kutoza kodi na kutumia fedha hizo, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango, ametaja kodi ambazo zitalazimika kukatwa.
Akizungumza na waandishi wa habari juzi kufafanua hoja ambazo hakuzielezea kwa kina bungeni, Dk Mpango alisema miongoni mwa kodi hizo ambazo baadhi ya wabunge na vyombo vya habari vilitetea zisikatwe ni pamoja na Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) katika utalii.
Nyingine ni kutoza kodi katika migahawa na maduka katika majeshi baada ya kufuta msamaha wake na kuhamisha jukumu la utozaji kodi za majengo kutoka halmashauri kwenda katika Mamlaka ya Mapato (TRA).
Akizungumzia VAT katika utalii, Dk Mpango alisema kodi hiyo haihusiani na ongezeko au kupungua kwa watalii nchini kwa kuwa watalii hao hawatazami kodi hiyo kama kigezo kikuu cha kwenda kuangalia vivutio vya utalii.
Alitoa mfano wa idadi ya watalii waliotembelea mbuga za wanyama kwa kipindi 2011 hadi 2014 katika nchi za Tanzania, Kenya na Afrika Kusini, ambayo inaonesha Tanzania licha ya kwamba haikuwa ikitoza VAT, bado ilitembelewa na watalii wachache kuliko nchi hizo ambazo zilikuwa zikitoza kodi.
Aliendelea kusisitiza kuwa mpaka kabla ya hotuba yake ya Bajeti ya Serikali ya 2016/17, nchi zote wanachama wa Jumuiya Afrika Mashariki zilikuwa zikitoza kodi hiyo kwenye huduma ya utalii isipokuwa Tanzania ambayo imependekeza kutoza katika bajeti yake ya mwaka 2016/17.
Kuhusu uamuzi wa serikali kuhamisha jukumu la kukusanya kodi za majengo kutoka katika halmashauri kwenda TRA, Dk Mpango alisema mamlaka hiyo ya kodi ndiyo yenye uzoefu wa kutosha katika ukusanyaji kodi za serikali na ndiyo yenye vituo vya ukusanyaji kodi katika wilaya na mikoa yote Tanzania.
Kuhusu viwango vya kodi ya majengo, alisema Waziri wa Fedha na Mipango ataweka viwango vya kodi ya majengo baada ya kushauriana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) ili kuweka uwazi na kujumuisha maoni ya wadau wote muhimu zikiwemo halmashauri husika.
Katika msisitizo mwingine alisema kuwa, mapato kutokana na kodi ya majengo yataingizwa katika mfuko mkuu ambao mawaziri wenye dhamana ya fedha na Tamisemi, ndio watakaoshauriana kuhusu mgawanyo wa fedha hizo kwa kuzingatia bajeti za halmashauri husika.
Kuhusu madai kwamba kuondolewa kwa misamaha ya kodi katika maduka na migahawa ya vyombo vya ulinzi na usalama kunaondoa motisha katika taasisi hizo, alisema uamuzi huo wa serikali upo palepale kwa kuwa misamaha hiyo ilikuwa ikitumika vibaya.
“Ili kuondoa kasoro hiyo, serikali imeamua kuweka utaratibu wa kuwalipa posho watumishi wa vyombo vya ulinzi na usalama ili wanufaike moja kwa moja kama walengwa. Kiasi cha posho atakayolipwa askari kitakokotolewa baada ya mashauriano na vyombo husika,” alisisitiza.
Kuhusu ushuru wa bidhaa kutozwa kwenye ada ya miamala ya uhawilishaji wa fedha, kama utaathiri mtumiaji wa mwisho, Dk Mpango alisema ushuru huo hautakatwa kwenye fedha zinazotumwa au kupokewa, bali katika ada inayotozwa na benki au kampuni ya simu.
Alifafanua kuwa kwa sasa sheria inatamka kwamba ada hiyo itatozwa katika kutuma fedha tu, hivyo baadhi ya kampuni za simu na benki zilikuwa zikitumia mwanya wa sheria hiyo kupunguza wigo wa kodi kwa kutoza ada wakati wa kupokea tu.
Categories: