Barabara za Dk. Magufuli sasa zatelekezwa Dar.

Posted by Unknown on 19:16 with No comments

  Baadhi ya barabara zilizokuwa zinajengwa jijini Dar es Salaam kwa lengo la kupunguza msongamano, ujenzi wake umekwama baada ya wakandarasi kuzitelekeza na kuondoa vifaa vyao.
Barabara hizo zilianza kujengwa mwanzoni mwa mwaka jana katika maeneo mbalimbali.
 
Waziri wa ujenzi, Dk. John Magufuli (pichani) mwanzoni mwa mwaka huu alizitembelea barabara hizo na kuweka mawe ya msingi, lakini kwa sasa hakuna shughuli yoyote inayoendelea eneo la ujenzi.
 
Uchunguzi uliofanywa na NIPASHE katika barabara ya Tangibovu hadi Goba katika Wilaya ya Kinondoni umbali wa kilomita tisa umebaini kwa sasa hakuna magari wala tingatinga eneo la ujenzi.
 
Aidha, kuanzia Goba hadi Mbezi Luis ujenzi umesimama kwa muda huku wananchi wakishindwa kujua sababu ya kazi hiyo kukwama.
 
Baadhi ya wananchi katika maeneo hayo wameshangazwa kuona magari na vifaa vingine vilivyokuwa vikitumika katika ujenzi huo kuondolewa wakati kipindi ambacho ujenzi ungefanyika vizuri kuliko kipindi cha mvua.
 
Barabara nyingine ambayo ujenzi umesimama ni ya Ubungo External kupitia Maji chumvi hadi Bonyokwa.
 
Pia inayotokea Tabata dampo hadi Kigogo na Wazo kupitia Tegeta A hadi Goba ambazo ujenzi wake ulipangwa kukamilika ndani ya miezi 12.
 
Mkataba wa ujenzi huo ulisainiwa Machi mwaka jana na wakandarasi waliambiwa wahakikishe wanakamilisha kazi hiyo katika kipindi walichokubaliana na serikali.
 
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara (Tanroads), Patrick Mfugale, akizungumza siku ya kusaini maktaba huo na Wakandarasi aliahidi kwamba kazi hiyo itakamilika kama mkataba unavyosema. 
 
Akiweka jiwe la msingi katika ujenzi wa barabara ya Mbezi Tangibovu hadi Mbezi Luis, Dk. Magufuli aliwataka wakandarasi kukamilisha kazi waliyopewa kwa wakati.
Categories: