NEC yakabidhi majina 50,000 kwa Polisi

Posted by Unknown on 17:54 with No comments



MKURUGENZI wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Kailima Kombwey amemkabidhi Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) majina 52,078 ya watu ambao wamejiandikisha zaidi ya mara moja kwenye daftari la kudumu la wapiga kura.
Orodha hiyo imepokelewa na Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Benedict Wakulyamba aliyemwakilisha IGP. Orodha hiyo imekabidhiwa ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya watu hao ambao wamevunja sheria ya uandikishaji wa BVR.
Alisema wamebaini majina hayo baada ya kuingiza taarifa za wapiga kura na mitambo kubaini alama za vidole.
Kombwey alisema miongoni mwa watu hao, wapo waliojiandikisha mara mbili na wengine wamejiandikisha mara saba kwa kutumia majina tofauti.
Akipokea majina hayo, Wakulyamba alisema watayafanyia kazi haraka iwezekanavyo ili wahusika waweze kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.
Wagombea matatani
“Leo naomba kumkabidhi IGP wa Polisi majina ya watu ambao wamejiandikisha zaidi ya mara moja ili wasakwe na wachukuliwe hatua za kisheria,” alisema Kombwey na kuongeza kuwa miongoni mwa watu ambao wamejiandikisha zaidi ya mara moja wamo wanasiasa ambao wanagombea nafasi mbalimbali za kisiasa katika uchaguzi mkuu ujao.
Alisema mitambo ya EMC V Block inayotumika ina uwezo wa kulinganisha alama milioni 16 kwa dakika moja.
Katika hafla hiyo waandishi walioneshwa watu ambao wamejiandikisha wengine wakibadilisha mifumo ya nywele, wengine nguo walizovaa pamoja na majina.
Mkurugenzi huyo alisema hadi sasa kesi 12 zimeshafunguliwa mahakamani na baadhi zimeshaisha na wahusika wamehukumiwa kati ya kifungo cha miezi sita hadi miaka miwili jela pamoja na kupigwa faini.
Alionya kuwa mtu ambaye atahukumiwa kifungo cha kuanzia miezi sita huyo hatakuwa na sifa ya kupiga kura na ataondolewa kwenye daftari hilo.
Pia alisema hatua inayofuata kwa sasa ni kubaini watu ambao wamejiandikisha wakati siyo raia wa Tanzania na amesema watafanikisha hatua hiyo baada ya kushirikiana na Idara ya Uhamiaji. Alisema pia watu ambao watakuwa hawajafikisha miaka 18 siku ya kupiga kura ambayo ni Oktoba 25 pia watawekwa pembeni.
Hata hivyo hakuweza kutoa takwimu za raia wa kigeni mbao wamebainika kujiandikisha kwenye daftari hilo. Pia hakutoa takwimu za watu ambao watakuwa hawajafikisha miaka 18 siku ya kupita kura. Hata hivyo alisema kwamba Tume inaendelea kufanya uchambuzi na itakapokuwa tayari itatoa taarifa.
Aidha waandishi wa habari wamehakikishiwa kuwa hakuna mwananchi ambaye amejiandikisha jina lake litakosekana kwenye daftari la kudumu la wapiga kura. Naibu Katibu wa Mkurugenzi wa NEC anayeshughulikia Tehama, Dk Sisti Cariah alisema kwamba taarifa za watu zimetunzwa katika maeneo sita.
Maeneo hayo ni fomu aliyojaza mpiga kura wakati anaenda kujiandikisha, flash, kwenye kompyuta mpakato iliyoko kwenye mashine ya BVR pamoja na kadi ya kuweka kumbukumbu (SD Card).
Alisema kwamba kama kuna taarifa za mtu zimekosewa wakati wa uandikishaji wana mfumo wa kutafuta fomu za mtu mmoja ndani ya dakika tatu ili kupata usahihi wa taarifa ya mpiga kura kama jina, jinsia na mengineyo.
Dk Cariah aliwahakikishia wananchi kuwa kumbukumbu zao ziko salama na hata kama litatokea janga la asili, kumbukumbu zote za wapiga kura zimehifadhiwa sehemu tatu tofauti jambo ambalo litafanya kazi za tume hiyo kuendelea hata kama kutatokea janga.
Uhakiki wa simu
Hata hivyo aliwataka wananchi waendelee kuhakiki taarifa zao kwa kutumia namba za simu na pale watakapokuta taarifa zao sio sahihi waende kwa Mkurugenzi wa Wilaya ili taarifa ziweze kufikishwa Tume.
Alikanusha uvumi kuwa utaratibu wa kutumia simu wa kuhakiki taarifa za mtu utamfanya mtu apige kura na kusisitiza kuwa upigaji kura utafanyika kwa mtu kwenda kituo cha kupigia kura na kuchukua karatasi ya kupigia kura na kupiga kura kisha kuitumbukiza kwenye sanduku
Categories: