Tofauti 15 kati ya Mrema, Lowassa
Posted by Unknown on 17:50 with 1 comment
Aliyekuwa
Mjadala uliopo katika jamii kwa sasa ni kufananisha ufuasi mkubwa anaopata Edward Lowassa baada ya kujiengua CCM na kujiunga na Chadema na alioupata Augustine Mrema alipojiunga na NCCR-Mageuzi mwaka 1995 akitokea CCM.
Wanajadili kuwa alipoangukia Mrema, ndipo atatumbukia Lowassa huku wakilinganisha umati wa watu unaomfuata Lowassa na ilivyokuwa enzi za Mrema; walivyopokewa na upinzani, vijana wanavyoonekana kuhamasika na kushindwa kuvunja mtandao wa CCM.
Ukweli ni kwamba kuna tofauti kubwa kati Mrema na Lowassa kama inavyoelezwa hapa chini:
Tofauti zao
Tofauti ya kwanza ni taswira yao katika jamii, kwamba Mrema alijijenga yeye binafsi ili aonekane kuwa nyota serikalini na katika jamii hasa aliposuluhisha masuala ya ndoa. Lakini Lowassa amekuwa kama taasisi iliyojengwa na wanasiasa na wafanyabiashara.
Mrema alijiondoa CCM ili asifukuzwe kwa utovu wa nidhamu aliouonyesha baada ya kutoa bungeni siri za Baraza la Mawaziri kuhusu kufisidiwa kwa mabilioni ya shilingi yaliyotolewa kwa ajili ya kufufua mkonge na alitumia hoja hiyo katika kampeni wakati wananchi walikuwa hawaamini. Lowassa amejiondoa baada ya jina lake kukatwa na vikao vya CCM bila kutoa sababu hivyo ikatafsiriwa kuwa ameonewa na amebeba ajenda tatu kubwa; kupiga vita umaskini, kutafuta ajira kwa vijana na kuimarisha elimu.
Mrema hakuwa na mawazo ya urais kabla ya kujiondoa CCM hivyo alipojiunga NCCR hakuwa na mikakati wala muda wa kujijenga kwa wananchi isipokuwa alitegemea umaarufu aliojijengea alipokuwa Waziri wa Mambo ya Ndani. Lowassa alianza kutamani urais mwaka 1995, aliposhindwa alisimamia mtandao uliomwingiza Ikulu swahiba wake Jakaya Kikwete na aliendelea kuutumia mtandao huo kujijenga akiwa na matumaini kuwa ndiye ataungwa mkono kumrithi Kikwete kwenye urais.
Mrema alijiunga na upinzani wakati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere alikuwa na nguvu na japokuwa alichangia kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi, hakutaka CCM ife akiwa hai, hivyo aliwaaminisha wananchi, kwa wakati ule, kwamba CCM ilikuwa bado chaguo bora. Lowassa amejiunga na upinzani wakati ambao Rais Kikwete anaonekana kukata tamaa hata kuitabiria kifo CCM na kwamba ikipona mwaka huu basi itakwenda na maji mwaka 2020.
Mwaka 1995 Mrema alipojiunga na NCCR ilikuwa takriban miaka mitatu tangu mfumo wa vyama vingi uruhusiwe hivyo vingi vilionekana kutokuwa na katiba nzuri, sera, taratibu wala mfumo mzuri wa uongozi na kukosa wafuasi wengi. Lowassa anajiunga wakati vyama vina ukomavu wa miaka 23; vina katiba, kanuni, sera, mfumo mzuri, viongozi madhubuti na wanachama wengi.
Alipokuwa CCM Mrema alipandikiza chuki dhidi ya upinzani akidai kuwa unaleta vita na chuki na haufai hivyo alipohamia upinzani alishindwa kubadili fikra hizo kwani CCM walitumia mikanda ya video iliyoonyesha vita katika nchi jirani ya Rwanda kuwatisha wananchi wasiwachague wapinzani. Lowassa hakukomoa upinzani ila alijenga ngome imara usiweze kupenya Monduli na amejiunga kipindi ambacho, wananchi wana uelewa mkubwa na wanajua vita husababishwa na viongozi au vyama tawala vinavyong’ang’ania madaraka hata vinapokuwa vimeshindwa.
Mrema alijiunga na upinzani wakati Watanzania hawakuwa wanajua faida na hasara zake, hivyo walikuwa wanaogopa, lakini Lowassa amejiunga na upinzani wakati jamii ina mwamko na hamasa kubwa baada ya kuona kazi iliyofanywa na wapinzani wachache bungeni na katika mabaraza ya madiwani, hivyo wengi sasa ni wanachama na mashabiki wa vyama vya upinzani na kwamba “iwe mvua au jua” wanataka mabadiliko.
Tofauti yao nyingine ni juu ya umuhimu wa ushirikiano. Mrema alipojiunga upinzani alikataa kuunganisha nguvu ili vyama vya upinzani vifanye kazi kwa ushirikiano na vimuunge mkono mgombea urais wa chama hicho, akidai NCCR ingesimama na kushinda uchaguzi peke yake. Lowassa amejiunga na Chadema wakati chama hicho kimekamilisha kujenga ushirikiano madhubuti na vyama vingine chini ya Ukawa na amesifu mikakati hiyo akisema ndiyo njia pekee ya kupambana na chama chenye mizizi mirefu kama CCM.
Kisiasa Mrema alikuwa maarufu kama kada lakini hakuwa na mizizi ndani ya chama ndiyo maana alipojivua uanachama na kujiunga NCCR hakuondoka na vigogo wala wanachama mashuhuri ili wamsaidie kuchukua nchi. Kwa upande wake, Lowassa ameonyesha nguvu zake; amewashawishi makada wengi kuhama CCM na kujiunga na Chadema kuanzia vijijini wakiwamo madiwani, wabunge na wenyeviti wa mikoa.
Tatizo jingine lililomkumba Mrema alipojiunga na upinzani ni hofu waliyokuwa nayo makada wa CCM juu ya uwezo wake kuongoza nchi na chama na kwamba alimudu alipokuwa Waziri wa Mambo ya Ndani kwa matamko yake au amri zake za kuwataka wanaomiliki silaha za moto isivyo halali nchini, wazisalimishe katika muda wa siku saba lakini alipwaya alipohamishiwa Wizara ya Kazi na Ajira. Lowassa amemudu wizara zote alizoteuliwa kuziongoza na kuonyesha kipaji cha uongozi kiasi cha kuelekea kumfunika hata bosi wake, Rais Kikwete katika kipindi cha miaka miwili ya uwaziri mkuu.
Kwa kuwa aliupa upinzani picha mbaya, alipohamia alipigwa mabomu ya machozi ili kumzuia na kuvuruga mikutano yake, kumfungulia kesi na kutisha wananchi waamini upinzani ni vurugu na ni vita. Lakini Lowassa anaingia upinzani wakati mazingira ya uhasama kati ya “ngunguri” na “ngangari” umepungua kiasi ndiyo maana Waziri wa Mambo ya Ndani, Mathias Chikawe amewasifu wapinzani walivyoandamana kumsindikiza mgombea huyo wa urais kwenda NEC kuchukua fomu huku wakisindikizwa na polisi.
Baada ya uchaguzi mkuu wa viongozi wa Bakwata kusuasua kwa muda mrefu, Mrema aliingilia na kuhakikisha unafanyika, pia alipenda kuvaa baraghashia ili ionekane hayuko mbali na watu wa dini zote. Lowassa alichafuliwa na sakata la Richmond hivyo alijiuzulu akarudi kwa wananchi kujisafisha kwa kushirikiana nao katika harambee za kuchangia vikundi vya kiuchumi (kama vicoba), madawati, ujenzi wa makanisa na misikiti matukio yaliyomjenga na hata kuwasahaulisha sakata la Richmond.
Mrema ameacha alama hadi leo; ujenzi wa vituo vidogo vya polisi karibu na makazi ya watu ili kupunguza uhalifu ingawa aligonga mwamba alipokwenda uwanja wa ndege wa Kimataifa kukamata dhahabu iliyokuwa inatoroshwa kimagendo, na kumzuia Oscar Kambona kurejea nchini. Lowassa husoma mazingira na sheria ndiyo maana aliweza kuzuia kubinafsishwa eneo la Mnazi Mmoja, Dar es Salaam; na alihakikisha inafutwa sheria ya kikoloni iliyotumiwa na Misri kuzuia Tanzania kutumia maji ya Ziwa Victoria, aliifurusha kampuni ya City Water kutokana na ubabaishaji, na shule za kata ambazo Serikali ya Awamu ya Nne inajivunia.
Mrema alipoingia upinzani aliwatisha sana watendaji wa serikalini kwamba NCCR-Mageuzi wakiingia madarakani makamanda kadhaa wa Jeshi la Polisi, viongozi serikali wangetiwa ndani. Lowassa amewaondoa hofu wote kwamba hana ugomvi, chuki wala kinyongo na akishinda hatalipiza kisasi.
Mwaka 1995 vijana wengi walijitokeza kumshabikia Mrema na kusukuma tu gari lake wakati wengi hawakuwa wamejiandikisha kupiga kura na waliojiandikisha hawakupiga kura. Lowassa amejiunga na upinzani wakati vijana wengi wamehamasika kujiandikisha kupiga kura na mijadala inayoendelea huenda wengi wakapiga kura ili kukamilisha kile wanachodai wanataka mabadiliko.
Categories: NEWS
Inafikirisha.Tukutane Oktoba25,2015.
ReplyDelete