Ahadi alizotoa Lowassa toka kuanza kampeni.

Posted by Unknown on 12:33 with No comments

Mgombea urais kwa tiketi ya Chadema, Edward Lowassa akiwapungia mkono wananchi waliojitokeza katika Uwanja wa Matarawe mjini Songea wakati wa mkutano wa kampeni uliofanyika karibuni. Picha ya Maktaba 

Dar es Salaam. Elimu bure hadi chuo kikuu, kuondoa umaskini, kuondoa ushuru wa mazao, kuweka riba kwa mazao yanayokopwa, ujenzi wa viwanda na kuongeza kasi katika utendaji kazi serikalini, ni mambo yaliyoibuka katika siku 10 za kampeni za mgombea wa Chadema, Edward Lowassa.
Mbunge huyo wa zamani wa Monduli, pia amekuwa akiahidi kujenga upya Reli ya Kati, kutafuta suluhisho la msongamano wa magari jijini Dar es Salaam, upatikanaji wa majisafi na kumaliza tatizo la umeme ndani ya mwaka mmoja kuwa ni mambo atakayofanyia kazi mara tu atakapopewa ridhaa ya kuongoza Taifa.
Lowassa, ambaye alikuwa Waziri Mkuu wa Kwanza wa Serikali ya Awamu ya Nne, pia amekuwa akiwatoa hofu wananchi kuhusu hali ya baadaye ya nchi iwapo CCM itaondolewa madarakani, huku akiwahimiza kujitokeza kupiga kura Oktoba 25.
Mgombea huyo, ambaye anaungwa mkono na vyama vya NCCR-Mageuzi, NLD na CUF ambavyo pamoja na Chadema, vinaunda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Jumatatu wiki hii jijini Dar es Salaam alihitimisha siku 10 tangu azindue kampeni zake Agosti 28 kwenye Viwanja vya Jangwani.
“Kipaumbele cha kwanza ni elimu, cha pili ni elimu na cha tatu ni elimu,” alisema Lowassa katika mkutano wa uzinduzi wa kampeni zake, akifafanua kuwa elimu ndiyo msingi wa kila kitu.
Mgombea huyo anayetumia kaulimbiu ya “mabadiliko”, licha ya kutumia muda mfupi katika mikutano yake ya kampeni, amekuwa akisisitiza umuhimu wa elimu na kuahidi kuondoa michango yote ya shuleni inayokwaza wananchi.
Lowassa alisema elimu bure itawezekana kwa kutumia mapato yatakayotokana na uzalishaji wa gesi, pamba na dhahabu.
Akiwa mkoani Tabora, Lowassa alitumia sehemu kubwa ya hotuba yake fupi kuzungumzia adha wanazopata wakulima.
“Kwa muda mrefu sasa wakulima wamekuwa wakikopwa bila hata riba. Hili nalo nalielewa. Nitalifanyia kazi,” alisema kwenye mkutano wa hadhara. “Lazima tuondoe vikwazo kwa wakulima, ikiwamo ushuru wa mazao ili waweze kuzalisha na kuuza kwa faida. Hawatakopwa tena, isipokuwa kwa riba.
“Chini ya utawala wa CCM, Tanzania ni nchi pekee ambayo wakulima wanakopwa tena na Serikali bila riba badala ya Serikali kuwalipa wakulima kama zinavyofanya nchi zinazothamini kilimo na ustawi wa wakulima. Ndiyo maana ninasisitiza Watanzania wachague.”
Lowassa alisema anaahidi kumaliza tatizo la umeme ndani ya mwaka mmoja sambamba na migogoro ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji huku akiahidi kuwa akiwa rais ataunda tume maalumu kumaliza suala hilo.
Aliahidi pia kuunda tume kuchunguza mgororo wa ardhi kati ya Kanisa la Efatha na wananchi na tume ya kutathmini utekelezaji wa maazimio ya Bunge kuhusu Operesheni Tokomeza Ujangili, ili kuwafidia wananchi waliopoteza ndugu, mifugo na mazao yao.
Lowassa amekuwa akieleza hayo ikiwa ni sehemu ya ilani ya Chadema na Ukawa iwapo wananchi watawapa ridhaa ya kuongoza nchi kwa miaka mitano ijayo.
“Tumetengeza ilani kiboko ambayo ndani ya miaka mitano, Tanzania yetu itabadilika. Lazima tupunguze tabaka kati ya tajiri na maskini kwa uchumi wa pamba, chai, dhahabu na gesi kwa nini tushindwe. Mkitupa ridhaa na Mungu akikubali tutakwenda kasi na tutakuwa na maendeleo,” alisema Lowassa.
Akiwa Bunju na baadaye Mbezi mkoani Dar es Salaam mapema wiki hii, Lowassa alisema hakutakuwa na muda wa kupoteza na kwamba mara baada ya kuchaguliwa ataanza mara moja kushughulikia ahadi zote, ikiwamo ya ujenzi wa viwanda kwa ajili ya kutatua tatizo la ajira.
“Nitajenga viwanda kukabiliana na tatizo la ajira,” alisema.
Pia, alisema akiingia madarakani, hakuna mgeni atakayefanya biashara nchini bila kuingia ubia na wazawa ili kuwajali vijana wa Tanzania.
Baada ya uzinduzi jijini Dar es Salaam, Lowassa, ambaye anaambatana na waziri mkuu mwingine wa zamani, Frederick Sumaye, ambaye amekuwa mzungumzaji mkuu, alifanya kampeni kwenye mikoa ya Iringa, Njombe, Ruvuma, Rukwa, Katavi, Kigoma, Tabora na baadhi ya maeneo ya mkoani Dar es Salaam.
Ahadi na maisha halisi ya wananchi
Katika karibu mikutano yake yote mikoani, Lowassa amekuwa akieleza kuwa CCM imeshindwa kubadilisha maisha ya Watanzania kwa zaidi ya miaka 50, hivyo ni wakati wa upinzani kufanya mabadiliko.
Amekuwa akitoa ahadi hizo mbele ya maelfu ya watu ambao wamekuwa wakijazana kwenye mikutano yake kila anapokwenda.
“Nakumbuka jinsi alivyopigania suala la uanzishwaji shule za kata, mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria na kumbana mkandarasi aliyekuwa akijenga Barabara ya Shekilango jijini Dar es Salaam. Ni mtu wa uamuzi, anaweza kutusaidia sana,” alisema Patrick Omendi, mkazi wa Songea mjini, Ruvuma.
“(Lowassa), Si mzungumzaji sana kama mgombea urais wa CCM, lakini sisi tunachokitaka ni mabadiliko tu kwa sababu Ikulu haendi kuzungumza, anakwenda kufanya kazi,” alisema Cyprian Kaijage, mkazi wa Kigoma.
Matumizi ya chopa
Lowassa, ambaye alizunguka karibu mikoa yote wakati akitafuta wadhamini ndani ya CCM kabla ya kuenguliwa, alianza kampeni zake mikoani kwa kutumia usafiri wa ardhini, lakini alianza kutumia usafiri wa anga kuanzia Songea na baadaye Katavi, Kigoma na Dar es Salaam.
Uamuzi wa kutumia ndege na hasa helikopta ulifanywa kwa ajili ya kuwafikia wananchi wengi katika muda mfupi.
Akizungumzia suala hilo, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema kutokana na ukweli kwamba kuna majimbo 265, ni vigumu kuyamaliza yote kwa kutumia magari ndani ya siku 60 zilizopangwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
Alisema akitumia chopa atafika katika majimbo 240, huku akitangaza kwamba wabunge machachari wa chama hicho watajigawa katika makundi manne kwa ajili ya kuzunguka mikoa mbalimbali kufanya kampeni kwa kutumia chopa nne.
Makada wa zamani CCM
Makada wengine wanaotumika kuishambulia CCM kabla ya Lowassa kuzungumza kwenye mikutano yake ya kampeni ni mwenyekiti wa zamani wa CCM mkoani Singida, Mgana Msindai, aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Hamis Mgeja na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Lawrence Masha.
Wengine ni aliyekuwa Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Goodluck Ole Medeye.

Categories: