Magufuli: Nitaondoa misamaha ya kodi

Posted by Unknown on 09:14 with No comments
Mgombea urais wa CCM, Dk John Magufuli akimnadi
Mgombea urais wa CCM, Dk John Magufuli akimnadi mgombea ubunge wa Jimbo la Bumbuli, January Makamba (kushoto) wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa Togotwe mjini Tanga jana. Picha na Adam Mzee wa CCM 
By Nuzulack Dausen
Tanga. Mgombea urais wa CCM, Dk John Magufuli amemaliza kampeni zake mkoani hapa, akiahidi kuwakaba koo wawekezaji wakubwa wanaonufaika na misamaha ya kodi isiyokuwa na tija kwa nchi.
Dk Magufuli alisema anataka Serikali yake iwe rafiki kwa wafanyabiashara wote, lakini wawekezaji wakubwa ni lazima waondolewe misamaha ya kodi isiyokuwa na tija ili fedha  zitakazopatikana zikasadie kuendeleza miradi mbalimbali ya Serikali.
Akiwahutubia wakazi wa Bumbuli wilayani Lushoto jana, Dk Magufuli alisema inasikitisha kuona badala ya wafanyabiashara wakubwa kubanwa kulipa ushuru, wafanyabiashara wadogo kama waendesha bodaboda na mama lishe wanaonewa.
“Nitakuwa upande wenu siku zote, sina maana Serikali yangu nitakayounda haitakusanya ushuru, lakini nitayabana makampuni makubwa ambayo hupewa tax holiday (msamaha wa kodi) kwa miaka mitano, ikiisha wanabadilisha jina na kupatiwa mingine mitano. Najua wananisikia huko waliko, ndugu zangu hao mimi nitalala nao mbele,” alisema huku akishangiliwa.
Akionekana kuongea kwa ukali, Dk Magufuli, ambaye amekuwa waziri tangu utawala wa Serikali ya Awamu ya Tatu, alisema: “Ni lazima walipe ushuru na kodi ili fedha zinakazopatikana zisaidie kuwasomesha watoto shule bure na kufidia ushuru kwa wafanyabiashara wa chini usio na kichwa wala miguu.”
Katika mkutano huo uliofurika watu na wengine kukaa kwenye miteremko ya milima, mbunge huyo wa Chato anayemaliza muda wake, alisema Serikali yake itakuwa makini kwa ajili ya watu na kutatua kero za masikini. Mgombea huyo aliyekuwa akimaliza mkoa wa nane kumwaga sera zake, aliwaahidi wakazi hao kutatua changamoto zilizopo katika kiwanda cha chai cha Mbonde ambacho hivi karibuni kilichukuliwa na Serikali baada ya kufungwa kutokana na mvutano baina ya mwekezaji na wakulima.
Hatua hiyo, alieleza kuwa ni moja ya mikakati yake ya kujenga viwanda vikubwa, vya kati na vidogo itakayochangia kukuza ajira kwa asilimia 40 na kuongeza bei ya zao la chai. “Tutawahamasisha watu wenye uwezo ndani ya nchi waanzishe viwanda vidogo vidogo ili vitoe ajira kwa vijana wetu,” alisema.
“Hii ndiyo maana tutaendeleza usambazaji umeme vijijini kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (Rea) ili usaidie kujenga viwanda vidogo vijijini ambavyo vitapunguza umasikini,” alisema. Kama ilivyo ada, Dk Magufuli aliahidi kujenga kwa lami barabara ya Soni hadi Bumbuli yenye kilomita 22. 89.
Kwa upande wake mgombea ubunge kupitia CCM jimbo la Bumbuli, Januari Makamba alisema kiwanda cha Mbonde kilishachukuliwa na Serikali na fedha zilishatengwa, lakini urasimu umechangia kuchelewesha kuanza kazi.
Januari aliwaonya Watanzania kutoharakia mabadiliko yasiyo na tija kwa kuwa kuna baadhi ya nchi kama Zambia ilifanya hivyo, lakini mpaka sasa haijaonja matunda ya mabadiliko bora. Mkazi wa Sunta mjini hapa, Khatibu Shelutete alisema ahadi nyingi za Dk Magufuli zinatekelezeka kwa kuwa historia yake katika kila wizara inaonyesha hufanya vizuri na huwa hana mchezo.
“Kwetu hapa kero kubwa ni hospitali na barabara ya kutoka Soni hadi hapa Bumbuli. Hii barabara ambayo leo Magufuli ameahidi tena alishawahi kuahidi Rais Kikwete alipoomba kura mwaka 2010, lakini hadi leo bado haijajengwa,” alisema Shelutete.
Dk Magufuli amekuwa akitumia sehemu kubwa ya mikutano yake kuwasihi wananchi kutowachagua wanasiasa wenye tamaa ya madaraka ambao mipango yao ya haraka haraka inaweza kuchochea kuvuruga amani nchini.
Alisema anapenda kuiongoza nchi yenye utulivu na amani ambayo wananchi wake hawagawanyishwi kwa dini, kabila au vyama.
“Naomba tuitunze amani yetu ndugu zangu. Hata Kenya wakati wa uchaguzi waliuana wao kwa wao, Rwanda kule watu wasiopungua milioni moja waliuawa, vivyo hivyo, kule Uganda na Burundi. “Niwaombe kura zenu Watanzania bila kujali dini zetu, makabila yetu, vyama yetu kwa sababu nataka kufanya kazi kwenye nchi yenye amani,” alisema.
Akiwa mjini Lushoto, Dk Magufuli aliahidi kuboresha masilahi ya wafanyakazi wote nchini kwa kuwapatia mishahara na kuwajengea nyumba ambazo miradi yake inaweza kufanywa na mifuko mikubwa ya hifadhi za Jamii kama NSSF na mingineyo.
Mwenyekiti wa CCM mkoani Tanga, Henry Shekifu alirusha vijembe kwa Waziri Mkuu wa zamani, Frederick Sumaye kuwa ni “mpiga dili” kuliko mgombea wa urais kupitia mwamvuli wa Ukawa, Edward Lowassa akimtuhumu kuwa alikula fedha za Shirika la Taifa la Hifadhi za Jamii (NSSF) na kumiliki maeneo makubwa ya ardhi mkoani Morogoro.
Katika kile kilichoonyesha yupo nyumbani, aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM, Yusuph Makamba kila aliposimama kuhutubia alitumia lugha ya Kisambaa kumwombea kura Dk Magufuli na kumponda Lowassa kuwa haifai kuwa rais akimtuhumu kwa rushwa na ufisadi.

Categories: