Maadhimisho ya Wiki ya wanawake Mwanza.

Posted by Unknown on 18:51 with No comments


Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Magessa Mulongo
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Magessa Mulongo 
Mwanza. Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Magessa Mulongo jana, aliwatolea uvivu wanawake kwa kuwaambia ni kikwazo cha kufikia lengo la asilimia 50 kwa 50 kutokana na ubinafsi, chuki, kukwamishana na kutosadiana.
Akihutubia kilele cha maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yaliyofanyika kimkoa eneo la Buhongwa jijini hapa, alisema wapo wanawake waliofanikiwa katika nyanja mbalimbali wanaopigania usawa kijinsia kati yao na wanaume hawawasaidii wenzao wanaohitaji msaada wao.
“Wanawake ndiyo mnaongoza kwa kuwekeana kauzibe pale mwenzenu anapojaribu kuinuka na kupiga hatua. Bila kubadilika lengo la 50 kwa 50 litakuwa ndoto isiyotimia,” alisema Mulongo.
Alitoa mfano wa tukio la hivi karibuni la mjamzito kukosa huduma katika Hospitali ya Wilaya ya Nyamagana iliyopo Butimba na Hospitali ya Mkoa wa Mwanza Sekou-Toure na wanawake wawili kupoteza watoto mapacha waliojifungua bila msaada wa madaktari na wauguzi, miongoni mwao wakiwamo wanawake wenzao.
Pia, alisema walimu wanawake katika Shule ya Sekondari ya Mihama katika Wilaya ya Ilemela mkoani hapa walifumbia macho vitendo vya walimu wanaume waliokuwa wakifanya ngono na wanafunzi wa kike hadi uchunguzi ulipobaini vitendo hivyo.
“Ili lengo la asilimia 50 kwa 50 lifikiwe lazima mjikane wenyewe kwa kujikosoa na kuacha kukwamishana miongoni mwenu,” alisisitiza Mulongo na kuwaacha midomo wazi viongozi wanawake wa mkoa huo waliomwalika.
Mkazi wa Igoma, Regina Sitta alisema baadhi ya akinamama huufumbia macho ukatili dhidi ya wenzao na watoto kwa kisingizio cha kuficha aibu ya familia.
Awali, akisoma risala kwa mgeni rasmi, Ofisa wa Shirika lisilo la kiserikali la Wadada Center for Solution Focused Approach, Anita Samson alisema licha ya jitihada zinazofanywa kupinga mila na desturi kandamizi, jamii nyingi nchini zinaendeleza kwa kisingizio cha mila na desturi.     

Categories: