Ombeni Sefue afunguka juu ya kusimamishwa kazi
Posted by Unknown on 11:15 with No comments
Baada ya kudumu Ikulu kwa takribani siku 127 zikiwamo 67 tangu aongezewe muda wa mwaka moja akiwa na Serikali ya Awamu ya Tano, Balozi Ombeni Sefue ameshukuru heshima aliyopewa na Rais John Magufuli kwa muda wote aliomsaidia kutekeleza majukumu yake ya ukatibu mkuu kiongozi na kueleza kuwa Serikali ya sasa ni ya mabadiliko.
Wakati Sefue akiondoka, mhandisi John Kijazi amepokea kijiti cha ukuu wa utumishi serikalini na kuahidi kuwa atafuatilia mazingira ya watumishi wote pamoja na mazingira yao, ili kurekebisha panapohitajika kwa lengo la kuongeza uwajibikaji na tija kwa wananchi.
Akizungumza muda mfupi baada ya kuapishwa kwa mrithi wake, licha ya kumshukuru Rais, Balozi Sefue aliwataka watendaji wote serikalini kumpa ushirikiano wa kutosha Balozi Kijazi ili kuleta ufanisi kwenye huduma za umma.
“Namshukuru Rais kwa kuniamini kwa kipindi chote nilichodumu naye. Ni heshima kubwa kuwatumikia Watanzania pamoja naye. Nitampa ushirikiano wowote atakaouhitaji katibu mkuu kiongozi mpya kwenye utekelezaji wa majukumu yake,” alisema Sefue.
Rais Magufuli, ameahidi na mara zote amekuwa akisisitiza adhma yake ya kutumbua majipu kwa watumishi wote ambao hawaendani na kasi yake.
Tangu taarifa za mabadilio hayo zilipotangazwa jana, kumekuwepo na tetesi nyingi kuwa huenda Sefue naye ni jipu lilikuwepo ikulu, suala ambalo halikupata maelezo ya kutosha kutoka kwa balozi huyo.
Alipoulizwa juu ya tetesi hizo alijibu kwa ufupi: “Hii ni Serikali ya mabadiliko.”
Kwa upande wake Kijazi, alisema atafanya kazi kwa kuzingatia vipaumbele vya Rais huku akimshauri namna sahihi za kuboresha mazingira ya utumishi serikalini.
Categories: NEWS
0 comments:
Post a Comment