UKAWA wawasha moto nje ya ofisi ya jiji.
Posted by Unknown on 12:27 with No comments
Dar es Salaam. Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), umesema hivi sasa hawataki kushtukizwa kuhusu tarehe ya uchaguzi wa kumpata meya wa jiji la Dar es Salaam na naibu wake, badala yake wapewe taarifa hiyo siku saba kabla.
Msimamo huo unafuatia viongozi wa Ukawa kutumiwa ujumbe mfupi na Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Sarah Yohana akiwataka wafike ofisini kwake kesho kuchukua majibu ya nini kinachoendelea juu ya uchaguzi huo ulioahirishwa mara tatu.
Machi 4, mwaka huu madiwani wa Ukawa walivamia ofisi za Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, kumshinikiza Yohana kuitisha kikao cha Baraza la Madiwani kwa ajili ya kufanya uchaguzi wa meya na naibu wake.
Hata hivyo, madiwani hao zaidi ya 20 hawakufanikiwa kuonana na Yohana aliyedai yupo nje ya ofisi kikazi, walimuachia maagizo ya kumtaka aitishe kikao hicho ndani ya siku saba. Maagizo hayo alipewa Ofisa Utumishi na Utawala, Iman Kasagara.
Akizungumza na Mwananchi kwa simu, Katibu wa Chadema Mkoa wa Dar es Salaam, Henry Kilewo alikiri kupokea ujumbe wa Yohana na kusema kesho wanakwenda ofisini kwa ajenda moja tu kuambiwa tarehe ya uchaguzi ambayo kisheria wanatakiwa kupewa siku saba za maandalizi.
“Wajumbe wote wa Ukawa tutakwenda keshokutwa (kesho), kumsikiliza mama Yohana. Lakini watambue kuwa hatutakubali waseme kuwa uchaguzi unafanyika kesho yake, hatutamkubalia kwa sababu sisi siyo watoto wadogo.
“Tukiona mambo hayaeleweki, siku hiyo hiyo tutajua nini cha kufanya kama Ukawa,” alisema Kilewo.
Alifafanua kwamba katika vikao vilivyopita halmashauri ya Dar es Salaam imekuwa na tabia ya kuwashtukiza, lakini safari hii hawatakubali mchezo huo, badala yake wanataka sheria ifuatwe ili uchaguzi huo ufanyike huru na amani bila figisufisu.
Akizungumzia kauli ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), George Simbachawene. Kilewo alisema haina tofauti na ile ya Yohana aliyewatumia ujumbe mfupi wa kuwataka waende ofisini kwake.
Juzi Simbachawene aliliambia Mwananchi kuwa, bado anaendelea kujiridhisha kuhusu zuio hilo kama batili au la, lakini ndani ya wiki hii atatoa mwelekeo wa uchaguzi huo.
Hali ilikuwa vivyo hivyo, kwa Yohana aliyemweleza mwandishi wa habari hii afike ofisini siku ya Jumatatu (leo), kwa maelezo zaidi juu ya sakata hilo.
Mara ya mwisho uchaguzi huo ulipangwa kufanyika Februari 27, lakini haikuwezekana kutokana na zuio la mahakama ambalo mwishoni, lilisababisha tafrani kati ya madiwani wa Ukawa na mwenyekiti wa uchaguzi huo,Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam, Theresia Mmbando.
Tafrani hiyo ilisababisha Mbunge wa Kawe, Halima Mdee na wa Ukonga, Mwita Waitara pamoja na madiwani watatu kumatwa na kufunguliwa kesi ya kumshambulia Mmbando mahakamani.
Categories: habari
0 comments:
Post a Comment