Waziri Mkuu azitaka benki kupunguza tozo

Posted by Unknown on 13:11 with No comments


Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amezitaka taasisi za fedha nchini kuangalia upya viwango vya gharama zinazowatoza wateja ili kuwawezesha wananchi wengi kunufaika na huduma hiyo.
Majaliwa alitoa rai hiyo jana mjini hapa wakati akifungua mkutano wa wadau wa Jumuiya ya Benki za Wananchi (Cobat).
“Pamoja na mafanikio yaliyopatikana katika sekta hii bado kuna changamoto ambazo wananchi wanakabiliana nazo ikiwamo gharama kubwa zinazotozwa katika huduma za fedha,” alisema.
Aliitaja changamoto nyingine kuwa ni huduma za fedha kutokidhi mahitaji ya walengwa, huduma zisizoridhisha na uelewa mdogo wa masuala ya fedha miongoni mwa wananchi.
“Kuna changamoto ya kutokuwapo kwa urari (usawa) wa taarifa mbalimbali na kuwapo kwa baadhi ya sheria na taratibu zinazokwamisha ufanisi wa kiutendaji wa baadhi ya taasisi hasa zile zinazolenga kuhudumia watu wa kipato cha chini,” alisema Majaliwa.
Waziri wa Fedha, Dk Philip Mpango alisema benki za wananchi ambazo zinaunda jumuiya hiyo hadi mwaka jana zilikuwa na mali inayofikia Sh86 bilioni na kutoa mikopo yenye thamani ya Sh56.2 bilioni kwa wateja wao.
“Changamoto iliyopo ni wananchi wengi wanaoishi vijijini kutopata huduma rasmi za kifedha na hiyo imebainishwa na utafiti uliofanyika nchini mwaka 2013, kuwa wananchi wanaopata huduma rasmi za kibenki ni asilimia 57.4 tu,” alisema.
Mwenyekiti wa Cobat, Elizabeth Makwabe alisema benki za wananchi zimekuwa zikifanya kazi ya kuwafikia waishio pembezoni. Alisema benki hizo zilizojiunga na umoja huo zipo 10 tu katika mikoa minane nchini. Pia aliwataka wadau wake kuhakikisha zinasambaa nchi nzima.

Categories: