Kodi ya petroli, dizeli, mafuta ya taa kuwasha moto bungeni leo.
Posted by Unknown on 11:28 with No comments

Sambamba na kujadili bajeti pia watajadili taarifa ya hali ya uchumi na mpango wa maendeleo wa taifa 2015/16, uliowasilishwa mwishoni mwa wiki na Waziri wa nchi, ofisi ya rais, mahusiano na uratibu, Dk. Mary Nagu.
Wakizungumza na NIPASHE kwa nyakati tofauti, Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila, alieleza maeneo yatakazua mjadala mkali ni pamoja na deni la taifa limefika Sh. trilioni 35 bila matokeo yoyote, kwani fedha hizo zingeweza kujenga reli ya kati na bandari.
"Kukopa siyo kosa ila ni lazima serikali itueleze ilikopa na kufanyia nini fedba husika," alisema.
Alisema shilingi ya Tanzania imeendelea kuporomoka dhidi ya Dola ya Marekani, huku Waziri wa Fedha, Saada Salum Mkuya, akieleza kuporomoka huko kunatokana na kuimarika kwa uchumi wa Marekani, lakini cha kushangaza safaru za nchi nyingine hazijaporomoka kama shilingi yetu. "Serikali imeshindwa kusimamia uchumi, ndiyo mana tunaagiza nje vitu ambavyo vikisimamiwa vitaagizwa nchini, inaonyesha usimamizi wa serikali nidhamu ya serikali ni ndogo," alisema.
Jingine ni kupanda kwa kodi ya mafuta ya petroli na diseli, na kwamba asilimia 40 ya uchumi wa dunia, mafuta yakipanda yanaathiri watu wa kawaida kwa kuwa bidhaa zitapanda mara dufu na kusababisha mfumuko wa bei.
Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Peter Msigwa, alisema pamoja na taarifa ya kambi rasmi ya upinzani hataunga mkono ongezeko la asilimia tano na kufanya asilimia 15 ya mapato ghafi ya taasisi na mashirika kuingia kwenye mfuko mkuu wa serikali.
Alitolea mfano Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa), ambalo linatakiwa kutumia mapato yake kwa ajili ya uhifadhi ambako kunahitaji fedha nyingi wakati mbunge wa Arumeru Magharibi (CCM), Goodluck ole Medeye, alisema hakubaliani na ongezeko la ushuru wa mafuta ya taa kwa Sh. 150, kwani kutaathiri wananchi wengi.
Wakati Waziri Mkuya akiwasilisha bajeti Juni 11, mwaka huu, alipotangaza ongezeko la kodi ya mafuta ya taa, petrol na diseli, wabunge waliguna na kuanza kunong'ona.
BAJETI YASUASUA
Wakati huo huo, utekelezaji wa bajeti ya Tanzania umeshindwa kufikia lengo kwa asilimia 12.7, kwa miaka minne mfululizo, kutokana na mapungufu ya ukusanyaji kodi na matumizi makubwa.
Akiwasilisha mada ya changamoto za mchakato wa bajeti katika ukusanyaji wa mapato na utatuzi, katika semina ya wabunge, Kamishina wa uchambuzi wa sera wa Wizara ya Fedha, Bedason Shallanda, alitaja kipindi hicho ni kuanzia mwaka wa fedha 2010/11 hadi 2014/15, iliandaliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Maendeleo (UNDP).
Categories: NEWS
0 comments:
Post a Comment