Prof. Lipumba apuliza kipenga urais Ukawa.

Posted by Unknown on 11:25 with No comments


Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Prof. Ibrahim Lipumba.
Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Prof. Ibrahim  Lipumba, amepuliza kipenga cha urais ndani ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kwa kuwa wa kwanza kuchukua fomu.
 
Ukawa unaundwa na vyama vya Chadema, NCCR-Mageuzi, NLD na CUF ambavyo vimekubaliana kusimamisha mgombea mmoja atakayepambana na mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba 25, mwaka huu.
 
Aidha, amewapiga vijembe makada wa CCM waliochukua fomu kuomba kuwania urais kupitia chama chao kwa kudai kuwa baadhi yao walistahili kuwa jela kutokana na ufisadi waliofanya lakini inashangaza kuona wamechukua fomu kuwania nafasi hiyo nyeti.
 
Prof. Lipumba alichukua fomu rasmi jana jijini Dar es Salaam na kukabidhiwa na Katibu wa CUF Wilaya ya Kinondoni, Mohamed Mkandu.
 
Kabla ya kuchukua fomu, Prof. Lipumba alisindikizwa na mamia ya wafuasi wa chama hicho kutoka makao makuu ya CUF yaliyopo Buguruni hadi katika ukumbi wa Ubungo Plaza.
 
Aliwasili saa 6:47 mchana akiwa anaongozwa na pikipiki na magari ya viongozi mbalimbali wa chama hicho na kulakiwa na wafuasi wa CUF waliokuwa na mabango yaliyokuwa na ujumbe tofauti.
 
Baada ya kuwasili aliingizwa kwenye chumba maalum na  kuchukulia fomu, huku ulinzi mkali ukiwa umeimarishwa na walinzi wa chama (Blue Guard) kwa kushirikiana na askari wa Jeshi la Polisi.
 
Wakati wa kuchukua fomu, Prof. Lipumba alisindikizwa na Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Shariff Hamad, Makamu Mwenyekiti wa CUF, Juma Duni Haji na Naibu Katibu Mkuu Bara, Magdalena Sakaya.
 
KIJEMBE KWA CCM 
Akizungumza na wafuasi wa CUF baada ya kuchukua fomu, Prof. Lipumba alisema inashangaza kuona baadhi ya makada wa CCM wakijiweka mbele kuwania nafasi ya urais badala ya kupelekwa jela kutokana na kashfa mbalimbali zinazowakabili.
 
“Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ilibainisha baadhi ya watu hao ambao hivi sasa wanawania urais ndani ya CCM kuhusika katika sakata la akaunti ya Tegeta Escrow, serikali imewakumbatia na kushindwa kuwachukulia hatua zozote za kisheria na matokeo yake wanataka kuingia ikulu,” alisema.
 
Alisema baadhi ya makada hao fedha walizochota kifisadi hivi sasa wanazitumia kutafuta wadhamini na kwamba akifanikiwa kuingia ikulu atawashughulikia wote.
 
“Nikipewa nafasi ndani ya Ukawa nikaingia ikulu sitakuwa na msalie mtume na mafisadi hawa... nitawashughulikia wote,” alisema huku akishangiliwa na mamia ya wanachama wa CUF. 
 
Prof. Lipumba alisema akifanikiwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Ukawa, atahakikisha anakuwa rais wa kwanza wa Tanzania kupata tuzo ya Mo Ibrahim kwa kuongoza nchi kwa uwazi, uwajibikaji na kupambana na ufisadi bila woga. Alisema kutokana na utaratibu uliowekwa katika vyama vinne vinavyounda Ukawa,  atakuwa tayari kumuunga mkono mgombea yeyote ndani ya Ukawa atakayependekezwa  kupeperusha bendera ya umoja huo.
 
Aliongeza kuwa mambo mengine atakayoyafanya akichaguliwa kuwa rais ni kufufua mchakato wa Katiba Mpya ambao umekwama kwa kuanzia pale ilipoishia Tume ya Mabadiliko ya Katiba kwa kuzingatia maoni yaliyotolewa na wananchi.
 
Alisema maoni ambayo yalitolewa na wananchi kwa Tume ya Warioba yalichakachuliwa na  kuondoa mambo ya msingi ambayo ikiwamo uwajibikaji, uadilifu na kwamba akiingia madarakani ni lazima ahakikishe yanazingatiwa.
 
“Pamoja na kazi nzuri iliyofanywa na Tume ya Warioba kuchukua maoni ya wananchi hasa ya kuwawajibisha viongozi kuhusu kuweka fedha nje ya nchi na kutaka viongozi kutoa ufafanuzi katika zawadi wanazopewa vyote vimechakachuliwa wakati tulitegemea hivyo ndivyo vingesaidia kuweka uwazi, mimi lazima nivirudishe,” alisema.
 
VIPAUMBELE VINGINE
Vipaumbele vingine alisema ni  kuimairsha sekta ya ajira kwa  kufufua viwanda, kuboresha miundombinu, kuboresha kilimo katika usindikaji mazao, kuboresha sekta ya afya hasa katika kuhakikisha wanawake, watoto wanapata lishe bora na kuboresha matibabu kwa wazee.
 
“Takwimu zinaonyesha kuwa watoto 100 kati yao 42 wamedumaa kwa kukosa lishe bora,” alisema.
 
Alisema kuwekeza kwa watoto ndiyo msingi wa kujenga taifa imara na kwamba atalisimamia hilo na kuhakikisha watoto wa kike wanapata fursa ya elimu na kudhibiti mimba za utotoni.
 
Aliongeza kuwa kama bandari ya Mtwara na Tanga zingeboresha zingetumika kuwa vituo vikuu vya biashara na viwanda ambavyo vingetengeneza ajira kwa vijana na kuimarisha usalama wa nchi.
 
Prof. Lipumba alisema zipo taarifa ambazo zimetolewa kwamba China inatarajia kuhamisha ajira milioni 90 kwenda nchi mbalimbali duniani, hivyo ni vema Tanzania ikatumia fursa hiyo kuboresha mazingira ya biashara kwa kuboresha viwanda na bandari ili inufaike na ajira hizo.
 
Aidha, Prof, Lipumba alisema kauli mbiu ya chama hicho inasema “2015 ni mwaka wa  maamuzi” na hivyo, akawataka wananchi kujitokeza katika daftari la kudumu la wapiga kura ili wafanye maamuzi sahihi katika siku ya uchaguzi, Oktoba 25 mwaka huu.
 
Lipumba alishawahi pia kuwa mgombea urais kupitia CUF katika chaguzi za miaka ya 1995, 2000, 2005 na 2010. 
 
MAALIM SEIF
Kwa upande wake, Maalim Seif alisema Tanzania hivi sasa iko tayari kwa mageuzi kwa kuwa wananchi wamechoshwa na utawala kandamizi unaofanywa na Serikali CCM na kwamba wanataka enzi mpya ya kuishi katika nchi isiyo na ubaguzi wa kipato.
 
Alisema rais ambaye Watanzania wanamtaka ni yule mwenye upeo mkubwa, atakayeweka fursa sawa kwa kila mtanzania, atakayetoa fursa kwa kila mtu kunufaika na raslimali za taifa, mwenye uwezo wa kujenga uchumi wa nchi yake na atakayeleta mawazo mapya.
 
“Tunamuondoa Rais Jakaya Kikwete, tunataka mtu ambaye ataleta mabadiliko, wapo watu wanaomiliki mabilioni ya dola nje lakini hapa watu wanakufa kwa njaa, naomba jibu,  hivi katika wale waliochukua fomu CCM kuna msafi?” alihoji kabla ya kujibiwa 'hakuna'.
 
Makamu Mwenyekiti wa CUF, Juma Duni Haji alisema hata ikitokea wananchi wakikipa chama tawala miaka 100 ya uongozi hakiwezi kuwatoa katika umaskini kwa kuwa kimekumbatia mafisadi.
Categories: