TAIFA STARS YATOKA SARE HUKU IKIAGA MASHINDANO
Posted by Unknown on 09:51 with No comments
TIMU ya soka ya Taifa, Taifa Stars jana ilitupwa nje ya michuano ya kuwania kufuzu Kombe la Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN), licha ya sare ya bao 1-1 dhidi ya Uganda, The Cranes mjini hapa.
Sare hiyo ya jana kwenye Uwanja wa Nakivubo umehitimisha safari hiyo baada ya kuwa Stars ilifungwa mabao 3-0 katika mechi ya kwanza Juni 20, mwaka huu, kwenye Uwanja wa Amaan mjini Unguja, Zanzibar.
Kwa matokeo hayo, Stars imetupwa nje kushiriki fainali hizo za mwakani nchini Rwanda kwa jumla ya mabao 4-1. Uganda sasa itacheza na Sudan kupata mshindi wa kwenda Kigali mwakani.
Stars jana ilikuwa chini ya makocha wazawa Charles Boniface Mkwasa na Hemed Morocco, ambao waliteuliwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), siku mbili baada ya kutimuliwa kwa Mholanzi Mart Nooij kutokana na matokeo mabaya katika kipindi cha mwaka mmoja alichoiongoza Tanzania.
Katika siku za mwisho akiwa na Stars, Mholanzi Nooij alifungwa mechi tano mfululizo zikiwamo tatu za michuano ya Cosafa ambazo Tanzania ilialikwa Afrika Kusini.
Pia alipoteza mechi ya kwanza ya kufuzu kwa fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2017 dhidi ya Misri, kabla ya kufungwa na Uganda mjini Unguja.
Stars jana ilikuwa ya kwanza kupata bao katika dakika ya 58 lililofungwa na John Bocco kwa penalti baada ya mchezaji wa Cranes kuunawa mpira wa kona uliopigwa na Simon Msuva.
Cranes inayofundishwa na kocha wa zamani wa Yanga, Milutin Sredjovic ‘Micho,’ ilisawazisha katika dakika ya 83 kwa bao la Kizito Keziron baada ya kutokea piga nikupige langoni mwa Stars.
Mechi hiyo ilianza kwa timu zote kushambuliana kwa zamu na iliwachukua dakika 18, Stars kuandika bao la kwanza lililofungwa na Msuva, lakini mwamuzi Djamal Aden Abdi wa Djibouti alilikataa kwa madai mfungaji alikuwa ameotea.
Stars iliendelea kuwashika wapinzani wao katika dakika 15 za mwisho za kipindi cha kwanza, lakini Bocco alionekana mzito mbele akishindwa kutoa uamuzi hasa anapokuwa na mpira, huku Deus Kaseke akianza kwa mchecheto mechi yake ya kwanza ya kimataifa, lakini kadri muda ulivyoyoma, alionekana kuimarika akijiamini.
Pia wachezaji wengine wageni katika timu, mshambuliaji Rashid Mandawa, beki Mwinyi Haji na kiungo Mudathir Yahaya walicheza vizuri na timu ilibadilika kiuchezaji ukilinganisha ilipokuwa chini ya Nooij.
Stars sasa inaelekeza nguvu katika mechi zijazo za Afcon 2017 wakati itakapoikaribisha Nigeria ‘Super Eagles’ jijini Dar es Salaam, Septemba 4, mwaka huu.
Stars: Ally Mustapha, Shomari Kapombe, Mwinyi Haji, Kelvin Yondani, Nadir Haroub, Frank Domayo/Said Ndemla, Msuva/Ramadhan Singano, Mudathir, Bocco, Mandawa/ Salum Telela na Kaseke.
Categories: SPORTS
0 comments:
Post a Comment