Warioba aipa angalizo CCM kumpata mgombea urais.
Posted by Unknown on 09:33 with No comments

Waziri Mkuu wa zamani, Jaji mstaafu, Joseph Warioba (pichani), amekiasa Chama cha Mapinduzi (CCM) kupitia kamati zake kuwa makini katika kutenda haki katika kumpata mgombea atakayepeperusha bendera ya urais katika Uchaguzi Mkuu, Oktoba 25 mwaka huu.
Amesema vinginevyo kuna uwezekano wa kutokea mgawanyiko mkubwa ambao pia utagusa wale wa nafasi za ubunge na udiwani.
Kauli hiyo uliungwa mkono na Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere (MNF), Joseph Butiku, katika mdahalo kuhusu umuhimu wa kuzingatia misingi ya umoja, amani na haki hasa katika kuelekea uchaguzi mkuu mwaka huu.
Mdahalo huo ulioshirikisha wananchi kutoka jijini Dar es Salaam, viongozi wa asasi na taasisi mbalimbali, wanasiasa na wasomi ulifanyika jana huku watoa mada wakisisitiza haki, amani, umoja na kupinga rushwa katika uchaguzi huo.
Jaji Warioba ambaye pia alikuwa Mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba nchini, alisema kwa sasa Taifa kimekumbwa na mgawanyiko wa matabaka makubwa katika maeneo ya kikabila, udini hivyo kukiuka misingi iliyoachwa na waasisi wa Taifa.
Alisema kabla ya uhuru, Tanzania ilikuwa katika matabaka matatu ya wazungu, wahindi na waafrika huku huduma zikitolewa kwa kuzingatia mfumo huo, lakini waasisi wa Taifa walichukua maamuzi magumu ya kuondoa hilo na kusimamia uhuru na haki.
“Mimi najua wanaokusanyika Dodoma wana kazi kubwa sana maana hao wote wametangaza nia, kila mmoja anatoa ahadi, swali ni mtu akitoa ahadi nje ya ilani ya chama itakuwaje, je, haki itatendeka?,”alihoji.
Alisema CCM ni taasisi kubwa ambayo inaweza kugawanyika ikiwa haki haitatendeka na kuendelea kusisitiza kuwa hali hiyo haitaishia katika uteuzi wa nafasi ya rais bali itasambaa hadi uteuzi wa nafasi ya ubunge na udiwani na kuwasihi wananchi kuchukua tahadhari.
Alisema kwa misingi iliyowekwa na wasisi wa Taifa, viongozi ni wale watakaozingatia uadilifu vinginevyo nchi inaweza kwenda kwenye mwelekeo mbaya na kuvunja umoja na amani ambavyo vilijengwa.
“Pamoja na mambo mengine viongozi watakaochaguliwa wana wajibu wa kulinda amani na kuzuia ubaguzi…amani imejengwa pale palipokuwa na haki sawa kwa wote, bila dhuluma na kuheshimiana, tufike mahala amani iwe zao la haki, Muungano wetu wa miaka 50 umeleta umoja, lakini leo kumekuwapo na mkanganyiko…kwa mfano mwanasheria mku kufukuzwa akijadili katiba. Kujenga Muungano pasipo haki, haiwezekani, ” alisisitiza.
Kwa upande wake, Butiku alisema haoni amani moyoni mwake anapoliona Taifa likiyumba huku vyama vya siasa kikiwamo CCM kikiwa chanzo kwa kutofuata taratibu na katiba za vyama vyao.
“Chama changu na vyama vingine, havifuati utaratibu, ni magwiji wa kuvunja katiba zao. Kwa mfano mwaka 1995, kuliundwa kundi la mtandao…waliamua kufanya kazi nje ya chama ambalo linaonekana lipo ndani ya CCM, lakini lipo nje ya chama, ajenda yao ilikuwa nje ya CCM….wakisema CCM ni chama cha mizengwe, kinatuchelewesha kupata maendeleo ya haraka,” alisema na kuongeza:
“Linatoka kundo nje ya chama, likijiita chama, likijificha ndani ya chama, wanavunja katiba ya chama….wote waliingia serikalini, wakaacha mgogoro wa chama, wakaanza kupigana.” Wagombe 38 si kitu, je, chama kiko wapi? Kama wenyeviti 15 wa CCM, wamefanya uchaguzi wao, Dodoma wanakwenda kufanya nini?”
Butiku pia alionya kuhusu rushwa kwani umeenea kila mahali huku wazee, vyombo vya habari na viongozi wakiwamo wa dini wakiingia huko na kusema huko ni kwenda nje ya utaratibu.
Categories: NEWS
0 comments:
Post a Comment