Wabunge Ukawa wawaweka viongozi kiti moto.
Posted by Unknown on 09:34 with No comments

Wabunge wa vyama vinavyounda Umoja wa Kutetea Katiba ya Wananchi (Ukawa) juzi waliwaweka kiti moto viongozi wao wakitaka masuala mawili ambayo hayajaamuliwa katika ushirikiano wao kufikiwa uamuzi haraka iwezekano.
Hali hiyo ilitokea juzi jijini Dar es Salaam wakati wabunge hao walipokutana na viongozi wao, wenyeviti wenza, Freeman Mbowe (Mwenyekiti Chadema); James Mbatia (Mwenyekiti NCCR-Mageuzi) na Profesa Ibrahim Lipumba (Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi- (CUF), walitaka viongozi hao wafikie uamuzi juu ya majimbo 13 ya ubunge ambayo hajaamuliwa na suala la atakayegombea urais kwa kofia ya Ukawa.
“Unajua wabunge wameonyesha kutokufurahishwa na kasi ya kufikiwa maamuzi. Kimsingi wamewataka viongozi hao wawe wamekwisha kuafikiana hadi ifikapo Jumamosi. Ni kama walipewa saa 48 hivi waamue,” kilisema chanzo chetu ndani ya kikao hicho kilichokuwa cha kuwekana sawa kuelekea uteuzi wa wagombea ubunge na mgombea urais.
Ukawa uliundwa na Chadema, NCCR-Mageuzi, CUF na NLD. Ulianza baada ya kukataa kubadilishwa kwa rasimu ya Katiba mpya iliyowasilishwa kwenye Bunge Maalum la Katiba na Tume ya Kurekebisha Katiba iliyoongozwa na Jaji Joseph Warioba mwaka jana.
Wajumbe wanaotokana na vyama hivyo chini ya mwavuli wa Ukawa, walisusia Bunge hilo kwa kile walichosema kuwa CCM ilikuwa inatumia wingi wa wajumbe wake kubadili maoni ya wananchi katika rasimu ya katiba mpya na hivyo kuweka yanayotetea maslahi ya chama chao.
Baada ya kususia Bunge la Katiba, Ukawa walikubaliana kwa pamoja kwamba ushirikiano wao ni wa kudumu na wataingia kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka huu kwa kuachiana majimbo, na nafasi ya urais watasimamisha mgombea mmoja.
Tayari ushirikiano huo umeshathibitika Zanzibar ambako kwa kiwango kikubwa CUF imeachiwa kusimamisha wagombea wake kwenye nafasi zote za ubunge na rais bila vyama hivyo kuweka wagombea.
Taarifa za awali ambazo zilitolewa na viongozi wa Ukawa Mei mwaka huu zilisema kuwa walikuwa wamekwisha kubaliana juu ya kuachiana majimbo kasoro 13 tu Tanzania Bara ambayo viongozi wake walikuwa wanaendelea na mazungumzo.
Hata hivyo, wakati viongozi wa Ukawa wakikuna vichwa, Profesa Lipumba aliibuka na kusema kuwa atawania tena urais mwaka huu. Kama atapitishwa na Ukawa itakuwa ni mara ya tano anagombea kiti hicho. Kwa mara ya kwanza aligombea mwaka 1995, kisha 2000, akajaribu tena 2005 na mwaka 2010 pia alirusha karata yake.
Kwa mara ya kwanza tangu kuanza tena kwa mfumo wa vyama vingi nchini mwaka 1992 na uchaguzi mkuu wa vyama vingi kufanyika mwaka 1995, vyama vya upinzani havijaungana kwa pamoja kusimamisha mgombea mmoja kama ambavyo inaelekea mwaka huu.
Habari kutoka ndani ya kikao cha Ukawa juzi zinasema kuwa baadhi ya wabunge waliwatisha viongozi wao kwamba kama hawataamua juu ya masuala hayo mawili hadi ifikapo kesho, basi watakwenda hadharani na kuwambia wananchi ni nani hasa anakwaza umoja huo ili waamue kwenye sanduku la kura juu ya wasaliti hao.
NIPASHE jana ilizungumza na Tumaini Makene, Ofisa wa Habari wa Chadema kutaka kujua hasa kilichozungumzwa kwenye mkutano wa juzi, na kama ni kweli wabunge waliwaweka kiti moto viongozi wao juu ya mambo hayo mawili.
Makene alisema kuwa ni kweli mkutano ulifanyika na ulikuwa wa maelewano makubwa.
Categories: NEWS
0 comments:
Post a Comment