Kikundi cha viongozi NCCR chapinga Ukawa

Posted by Unknown on 18:23 with No comments


Wenyeviti wa baadhi ya vyama vinavyounda UKawa

Wenyeviti wa baadhi ya vyama vinavyounda UKawa 

Dar es Salaam. Makamu mwenyekiti wa NCCR Mageuzi, katibu mkuu na baadhi ya wajumbe wa Kamati Kuu wametangaza mapambano ya ndani ya chama hicho, wakipinga utekelezaji wa makubaliano ya vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kwenye Uchaguzi Mkuu.
Viongozi hao, ambao walisema wataendelea kuwaunga mkono wagombea wa chama hicho, pia wamemtaka mwenyekiti wao, James Mbatia kuitisha vikao kujadili mustakabali wa chama.
Viongozi wa Ukawa, ambayo pia inaundwa na Chadema, NLD na CUF, wamekubaliana kwa maandishi kusimamisha mgombea mmoja kuanzia ngazi ya urais hadi udiwani, lakini viongozi hao wa juu wa NCCR-Mageuzi waliwaambia waandishi wa habari jana kuwa makubaliano hayo hayajatekelezwa ipasavyo.
Akizungumza na waandishi wa habari kwenye mkutano uliofanyika Hoteli ya Landmark jana jioni baada ya kuahirishwa mara kadhaa, makamu mwenyekiti wa chama hicho, Leticia Ghati alisema hawana mpango wa kujiondoa Ukawa wala kuacha harakati za kuiondoa CCM , bali wanapinga ubabe wa Chadema kwenye mchakato wa uchaguzi.
Alisema mwaka 2010, NCCR ilisimamisha wagombea kwenye majimbo 67, lakini ndani ya Ukawa wamepewa majimbo 12 tu, wakati NLD imepewa majimbo matatu, lakini bado Chadema wamewaingilia.
Alisema Ukawa wameshindwa kushughulikia migogoro ya vyama, kushindwa kuzisimamia kamati za majimbo na kupata muafaka wa kuachiana majimbo.
Akifafanua msimamo uliotangazwa na Ghati, katibu mkuu wa NCCR, Mosena Nyambabe alisema Chadema wameteka Ukawa kwa kufanya kila kitu, ikiwamo hadi picha za kutangaza umoja huo.
“Sisi kama viongozi tumeona tuliweke hili wazi, tutawaunga mkono wagombea wetu katika kila ngazi kuhakikisha wanashinda. Hatujiuzuru lakini tunamtaka mwenyekiti wetu James Mbatia aitishe vikao kujadili mustakabali wa chama chetu, ”alisema Nyambabe.
Tangu jana mchana, ofisi ya makao makuu ya NCCR-Mageuzi imekuwa ikikanusha kuwapo na mkutano na waandishi wa habari.

Categories: