Sumaye asema Dk Magufuli amepoteza dira, anadandia
Posted by Unknown on 18:26 with No comments


Freederick Sumaye
Simiyu. Siku moja baada ya Dk John Magufuli kupachika jina lake kwenye operesheni ya Chadema ya M4C, Waziri Mkuu wa zamani, Frederick Sumaye amemuelezea mgombea huyo urais wa CCM kuwa ni mtu anayedandia hoja baada ya kupoteza dira.
Wakati akipewa majibu hayo, DK Magufuli alikuwa akiendelea na kampeni mkoani Kigoma, ambako ajenda yake kuu ilikuwa ujenzi wa barabara, huku mgombea wa Ukawa, Edward Lowassa akichanja mbuga mkoani Shinyanga.
Akiwa mkoani Kigoma jana, Dk Magufuli aliwaambia wananchi kuwa kirefu cha nembo ya M4C ni Magufuli for Change, badala ya Movement For Change, ambayo imekuwa ikitumiwa na Chadema kwa miaka takriban sita sasa, ikimaanisha “vuguvugu la mabadiliko”.
Dk Magufuli alisema yeye ndiyo mtu sahihi wa kuongoza mabadiliko na hivyo alama hiyo inatakiwa iwe na jina lake.
Lakini jana, Sumaye, ambaye ameingia Ukawa bila ya kujihusisha na chama chochote kati ya vinne vinavyounda umoja huo, jana alisema kauli hiyo ya Magufuli inaonyesha jinsi yeye na chama chake wanavyotapatapa.
“Ni aibu kubwa,” alisema Sumaye ambaye amekuwa mzungumzaji mkuu kwenye mikutano ya kampeni ya Lowassa.
“Yaani ni kama mtu anayezama baharini halafu maji yameanza kumuingia puani na kushindwa kupumua. CCM inazama na sasa inaanza kushika kila mahali kama mtu anayezama katika maji.”
Sumaye alisema hayo jana kabla ya Lowassa kupanda jukwaani kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Uwanja wa Malambo wilayani Bariadi mkoani hapa.
Akimchambua mgombea urais wa CCM, Sumaye alisema kauli yake imeonyesha jinsi asivyokuwa na aibu na imedhihirisha jinsi alivyopoteza dira kwa kudandia hoja na mipango ya wapinzani.
“Sisi tunadai mabadiliko na kama na dawa ya kunguni ni kukitoa kitanda na kukitupa nje wakaozee huko,” alisema Sumaye huku akishangiliwa na wananchi.
Lowassa
Kwenye mkutano huo, Lowassa aliyepokewa na maelfu ya wananchi waliokuwa wakimsubiri, aliahidi kumaliza kero ya maji kwenye wilaya kwa kuendeleza mradi wa kutumia maji ya Ziwa Victoria lililopo umbali wa kilomita 30.
Mbunge huyo wa zamani wa Monduli alifika eneo hilo saa 10:00 jioni na kukimbiliwa na wananchi waliotaka kumshika na kusababisha polisi kutumia nguvu ya ziada kuwazuia. Akizungumza na wananchi wa Bariadi, Lowassa alirudia tena ahadi yake ya elimu ya bure akisema kuanzia Januari mwakani hakuna mwanafunzi atakayelipa ada kuanzia darasa la kwanza hadi chuo kikuu.
Pia aliahidi kuboresha kilimo ili kiwe cha kisasa na cha kibiashara, huku akisisitiza msimamo wake kuwa Serikali yake haitamvumilia mtu atakayeshindwa kwenda na kasi yake.
Mgombea huyo pia alifanya mikutano mingine Maswa na Busega.
Dk Magufuli na barabara, reli
Mkoani Kigoma, Dk Magufuli Serikali yake itashirikiana na nchi jirani ili kuhakikisha wananchi wa mikoa ya mipakani wanapata fursa za kibiashara katika nchi hizo.
Akizungumza kwa nyakati tofauti na wananchi wa majimbo ya Manyovu, Kasulu Mjini na Muhambwe, Dk Magufuli alisema nchi za Burundi, Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) ni fursa kubwa ya kibiashara kwa wananchi wa Kigoma na mikoa mingine ya mipakani.
Akiwa katika jimbo la Manyovu, wilaya ya Buhigwe, Dk Magufuli alisema uchumi wa mkoa wa Kigoma utakuwa kwa kasi endapo fursa za kibiashara zitafunguliwa na kuwawezesha Watanzania kupeleka bidhaa zao nchi jirani.
Dk Magufuli alisema atahakikisha anajenga barabara ya Manyovu hadi Kasulu na ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kimataifa.
“Nitahakikisha tunaanzisha ushirikiano wa kibiashara kati ya nchi yetu na wenzetu wa Congo, Burundi na Rwanda. Watu wa Kigoma mtaweza kufanya biashara na nchi jirani na kuleta maendeleo kwa taifa letu,” alisema mgombea huyo.
Mgombea huyo alisisitiza suala la amani na kuwataka wananchi kutoa taarifa kwa vyombo vya usalama wanapowaona watu hatari hasa kutoka nchi za kigeni.
“Hakuna haja ya basi linalotoka Kigoma kwenda maeneo mengine kusindikizwa na polisi, Tanzania ndiyo kisima cha amani. Hatuwezi kuwa kisiwa cha amani kama mtaendelea kuwaficha wahalifu kwenye maeneo yenu,” alisema mgombea huyo.
Categories: NEWS
0 comments:
Post a Comment