Amani ya Burundi kusakwa Uganda

Posted by Unknown on 11:18 with No comments





Rais wa Uganda, Yoweri Museveni      
Rais wa Uganda, Yoweri Museveni       

Kampala, Uganda. Rais wa Uganda, Yoweri Museveni anatarajia kuendesha mazungumzo ya kutatua mgogoro nchini Burundi Desemba 27. Mazungumzo hayo pia yamepangwa kufanyika mjini Arusha nchini Tanzania.
Waziri wa Ulinzi wa Uganda, Crispus Kiyonga alisema Rais Museveni ataendesha mazungumzo hayo yatakayohudhuriwa na pande zinazopingana nchini humo.
Julai mwaka huu Rais Museveni alimuagiza Rais wa Burundi, Pierre Nkurunziza kuitisha mazungumzo yanayolenga kumaliza mgogoro huo unaoendelea nchini mwake na kusababisha vifo vya mamia ya raia huku wengine wakikimbilia katika nchi za jirani.
Waziri Kiyoga alisema masuala muhimu yanayotakiwa kutatuliwa kwenye mazungumzo hayo ni pamoja na kuunda Serikali yenye mshikamano, usalama na utulivu wa nchi hiyo.
Katika hatua nyingine, viongozi wa Burundi wamekanusha uwezekano wa kutokea mauaji ya halaiki nchini humo.
Mtandao mmoja wa habari uitwao Africa Time umeripoti kuwa japokuwa wasiwasi wa kimataifa kuhusu uwezekano wa kutokea mauaji ya umati nchini Burundi unaongezeka, lakini viongozi wa Bujumbura wamesisitiza kuwa hakuna uwezekano wowote wa kutokea mauaji kama hayo.
Huku hayo yakiripotiwa, Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika wiki iliyopita lilipitisha azimio la kuunga mkono uingiliaji wa kijeshi nchini Burundi kwa ajili ya kuwalinda wananchi wa nchi hiyo.
Azimio hilo ambalo inabidi lipitishwe pia na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, linasisitizia kupelekwa wanajeshi 5000 wa kimataifa mjini Bujumbura kulinda amani na kudhibiti kuendelea kutokea kwa vitendo vya uvunjifu wa amani na mauaji ya raia wasiokuwa na hatia.
Baraza hilo limewapa viongozi wa Burundi muda wa hadi kesho wawe wamekubaliana kuhusiana na mazungumzo hayo ili kurejesha amani.     

Categories: