Bomoa bomoa yasitishwa

Posted by Unknown on 16:23 with No comments


 0.2k
 Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kushirikiana na Baraza la Taifa la Hifadhi ya Mazingira (Nemc), imesitisha ubomoaji wa nyumba zilizojengwa katika Bonde la Mto Msimbazi ili kuwapa nafasi wakazi kuhama na kuokoa mali zao.
Bomoabomoa hiyo imewakumba watu wanaoishi mabondeni, kwenye kingo za mito, maeneo ya wazi na kwenye fukwe na imekuwa ikilalamikiwa na wakazi wanaoishi maeneo hayo, wakisema hawakupewa muda wa kujiandaa kuhama.
Waziri wa Ardhi, William Lukuvi alisema jana kwenye mkutano na waandishi wa habari ambao pia ulimuhusisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia Mazingira, January Makamba.
Lukuvi alisema kumekuwapo na malalamiko mengi dhidi ya ubomoaji wa nyumba na hivyo wameamua kutoa muda kwa wananchi hao kuondoa vitu vyao kuanzia jana hadi Januari 5 mwakani.
Alisema baada ya muda huo, bomoabomoa itaendelea kwa nguvu kwa wavamizi wote wa mabondeni, maeneo ya wazi, fukwe, kingo za mito na hifadhi za barabara.
“Kama unafahamu umejenga nyumba yako kwenye maeneo yasiyoruhusiwa kisheria tafadhali vunja mwenyewe kwa kuwa bomoabomoa itarudi kwa nguvu ,” alisema.
Lukuvi alisema jumla ya nyumba 8,000 zinatakiwa kubomolewa kwenye Bonde la Msimbazi na hadi sasa tayari nyumba 353 zimebomolewa.
Alisema katika kipindi hiki ambacho bomoabomoa imesitishwa, wataalamu wa wizara watakuwa wakipita kuwaelimisha wananchi faida ya kubomoa kwa hiari.
“Ukibomoa mwenyewe unaweza kuondoka salama na vyombo vyako, mabati, milango, madirisha hata matofali, lakini ukisubiri, vyote hivyo vitaharibiwa,” alisema.
Alisema baada ya Januari 5, ubomoaji utaendelea kwenye Bonde la Msimbazi, Mlalakuwa, Mbezi Beach na Kawe kabla ya kuhamia maeneo mengine.
Lukuvi alisema Sheria ya Mipango Miji namba 8 ya mwaka 2007 na Sheria ya Mazingira namba 4 ya mwaka 2004, zinakataza kujenga kwenye maeneo hatarishi kama Bonde la Msimbazi.
Akizungumzia eneo la Msimbazi, Lukuvi alisema linaandaliwa kwa ajili ya burudani kwa ajili ya wakazi wa Dar es Salaam.
Alisema bonde hilo lenye hekta 1,927 litakuwa kwa ajili ya burudani na kwamba awamu ya kwanza ya ujenzi itaanzia Salender Bridge hadi Vingunguti wakati awamu ya pili itaanzia Vingunguti hadi Pugu.
Kuhusu uvamizi wa viwanja, Lukuvi alisema kuanzia Januari mwakani wizara yake itatoa ramani za mitaa kwenye ofisi za Serikali za Mitaa ili watendaji waweze kusimamia uvamizi wa maeneo.
“Watendaji wakipewa ramani za mitaa yao watayafahamu maeneo ya wazi na zinakopita barabara na hivyo kuwa rahisi kuchukua hatua dhidi ya wavamizi,” alisema Lukuvi. Kwa upande wake, Makamba alisema tatizo la uharibifu wa mazingira limekuwa na athari kwa maisha ya binadamu.
Alisema watu wanavamia vyanzo vya maji na kujenga nyumba huku wengine wakikata miti ovyo.
Makamba alisema hekta milioni moja za miti zinakatwa kila mwaka, jambo ambalo linatishia nchi kuwa jangwa.
Alisema kuanzia mwakani, wizara yake itachukua hatua za kisheria dhidi ya watu wanaojenga kwenye kingo za maji, fukwe na kwenye vyanzo vya maji.
“Hatutamwangalia mtu usoni tutavunja majumba yote ambayo yamejengwa kinyume na Sheria ya Mazingira, hatutajali huyu ni kigogo au la,” alisema Makamba.
“Serikali ya Awamu ya Tano haitanii kama umevunja sheria kwa kujenga jengo kwenye maeneo yasiyoruhusiwa, bomoa mwenyewe ukishindwa tutakuja na tingatinga,” alisema Makamba.
Katika hatua nyingine, Naibu waziri wa wizara hiyo, Luhaga Mpina ameipa Nemc siku 30 kuhakikisha inatoa vyeti 512 vya tathmini ya athari kwa mazingira kwa wawekezaji waliotuma maombi yao muda mrefu.
Mpina alisema wawekezaji wamekuwa walilalamikia ucheleweshwaji huo ambao huchukua hadi miaka mitatu jambo ambalo ni kinyume cha sheria.
“Sheria inataka mdau aliyetuma maombi apate cheti chake ndani ya siku 90, lakini ninyi mnachelewesha. Sasa nataka hao wanaotakiwa kupata vyeti vyao wapate haraka,” alisema Mpina jana wakati wa ziara yake ya kikazi ofisi za Nemc.     

Categories: