Going Bongo ilivyotikisa Dar
Posted by Unknown on 17:00 with No comments

Jumamosi hii nilipata bahati ya kwenda kuangalia filamu ya Going Bongo kwenye jumba la sinema la Century Cinemax lililopo Mlimani City jijini Dar es Salaam.
Going Bongo ni filamu pekee iliyochezwa na Watanzania, inayooneshwa hapo. Kwa wiki hii filamu zingine zinazooneshwa ni pamoja na The Peanut Movie, The Good Dinosaur, Tamasha, Spectre, Hate Story 3, In The Heart of The Sea na zingine.
Mimi niliangia kuangalia Going Bongo kuanzia saa mbili usiku, ikiwa ni siku ya pili tangu ianze kuoneshwa kwenye theatre hiyo. Awali ya hapo, Ernest Napoleon, muigizaji mkuu wa filamu hiyo alinieleza kuwa show za Ijumaa zilikuwa karibu sold-out kwa maana ya siti takriban zote kujaa watu.
Watanzania wengi walikuwa na hamu ya kuthibitisha kama kuna utofauti wowote katika ya filamu hiyo na zingine za Tanzania. Utofauti ni mkubwa hasa kwakuwa imeigizwa Marekani na Tanzania, inachekesha, ina ubora mkubwa (haina tofauti na filamu za Hollywood) na ina kisa cha kusisimua.
Ni filamu nzuri inayoonesha kisa cha dakrari kijana aitwaye Lewis Burger (Ernest) anayejitolea kuja Tanzania kutoa huduma ya afya kwa mwezi mmoja.
Anapokuja Dar anapata shida sana kufika Sinza Mori alikotakiwa kufikia, kwanza anajikuta akienda Makongo na kuingia kwenye nyumba tofauti na kujikuta akifukuzwa kama mwizi.
Anapoipata nyumba yenyewe, anakuta mazingira magumu, nyumba anayoishi haina umeme na joto linamsumbua. Kituo cha afya anachoenda anakuta huduma ni mbovu, wagonjwa ni wengi na madaktari ni wachache.
Burger anajikuta akigeuka kuwa kituko hospitalini hapo na hali za wagonjwa zinamkosesha raha. Anajitahidi kufanya kila awezalo lakini anashindwa kufanya yote.
Mwishowe mchumba wake wa Marekani waliokuwa wamepanga kufunga ndoa anakuja Dar kwa kushtukiza kumfuata baada ya kuona amechelewa. Anaporudi Marekani, moyo wake bado unabaki kufikiria hali ya hospitali ile na madaktari wenzake.
Anaamua kuuvunja uchumba na mpenzi wake mrembo na kurudi tena Dar.
Ndani kuna waigizaji wengine wa Tanzania wakiwemo Mzee Chilo na Evans Bukuku. Kuna waigizaji wengine wa Marekani na wa Kenya pia.
Wakati naangalia filamu hiyo si mimi tu niliyejikuta nikicheka kwa vituko vyake, bali mke wangu pia mbavu zilimuuma. Watu wengine waliokuwemo humo walisikika wakicheka bila kikomo. Ni filamu nzuri na iliyoigizwa kwa ustadi mkubwa. Kila mtu alitoka ndani moyo wake ukiwa mweupe na kuisifia filamu hiyo.
Hiyo imenifanya nigundue kuwa inawezekana kabisa filamu za Bongo movies zikaanza kuoneshwa kwenye majumba ya sinema. Cha msingi ziwe na ubora na zipendwe na watazamaji.
Ziwe na visa vya kusisimua na vyenye uhalisia. Waigizaji wasiigize tu bali waishi kwenye filamu hizo. Ninaamini kama ubora wa filamu zetu ukiboreshwa, tasnia yetu ya filamu itapiga hatua na wadau watapata faida zaidi kuliko kutegemea mauzo ya DVD peke yake ambayo kwa sasa yamepungua sana.
Categories: celebrity

0 comments:
Post a Comment