CCM Moshi kumweka JPM mikononi mwa Mungu
Posted by Unknown on 19:03 with No comments


Rais John Magufuli
Moshi. Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa Kilimanjaro leo kimeandaa maombi maalum ya kumuombea Rais John Magufuli na wasaidizi wake kwa kujitoa mhanga katika kutumbua majipu.
Rais Magufuli amekaririwa mara kadhaa akiomba Watanzania kumuombea ili aendelee kuwashughulikia wote wanaofanya ufisadi na ubadhirifu, kula rushwa na wizi wa fedha za umma.
“Nataka niwahakikishie, nitaendelea kutumbua majipu yote mpaka yaishe na naomba mniombee ili kazi hii ifanyike kwa mafanikio,” Rais Magufuli amekuwa akisema katika baadhi ya hotuba zake.
Katibu wa CCM Mkoa Kilimanjaro, Deogratius Rutta alisema katika siku 100 za Rais kuwapo madarakani, amefanyia kazi mambo sita muhimu.
“Maombi hayo yatatanguliwa na maandamano ya wananchi yatakayoanzia ofisi ya CCM Mkoa hadi stendi kuu ya mabasi, viongozi wa madhehebu yote wataongoza maombi,”alisema.
Mambo ambayo CCM Kilimanjaro imekunwa nayo ni pamoja na Rais kujitoa mhanga na kuwa mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya ufisadi na wezi wa mali ya Taifa.
“Amebana matumizi ya Serikali yasiyokuwa ya lazima kama vile sherehe za siku ya Uhuru, kuwaapisha wabunge na safari za nje zisizokuwa na tija kwa taifa,” alisema Rutta.
Mambo mengine aliyoyafanya Rais kwa mujibu wa Rutta, ni kusimamia utoaji wa elimu bure kuanzia chekechea na kusimamia makusanyo ya mapato kutoka Sh900 bilioni hadi Sh1.4 trilioni kwa mwezi.
“Pia, ametumbua majipu kwa kuwafukuza na kuwawajibisha maofisa wa taasisi za umma waliohusika na tuhuma mbalimbali hasa ubadhirifu wa mali ya umma na uzembe kazini,” alisema Rutta.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa Kilimanjaro, Koka Moita alipoulizwa kama maandamano hayo ya CCM yana kibali, alisema hana uhakika kama wasaidizi wake wameyapokea kwa vile alikuwa vikaoni.
0 comments:
Post a Comment