TAKWIMU: MATOKEO KIDATO CHA NNE

Posted by Unknown on 13:51 with No comments


Dar es Salaam. Mfumo uliorejeshwa wa kupanga matokeo ya mtihani ya kidato cha nne kwa madaraja umeonyesha kushuka kwa kiwango cha ufaulu kwa asilimia 1.85, kwa mujibu wa matokeo yaliyotangazwa jana na Baraza la Mitihani la Taifa (Necta).
Pia matokeo hayo yanaonyesha Shule ya Sekondari ya Kaizerege ya mkoani Kagera imeshika nafasi ya kwanza kitaifa, ikiwa moja ya shule nne za Kanda ya Ziwa zilizo kwenye orodha ya kumi bora, ambayo imetawaliwa na shule binafsi.
Katika orodha ya kumi bora ya watahiniwa, wasichana wawili, akiwamo mmoja raia wa China, kutoka shule za Canossa (Butogwa Charles Shija) na Fedha Girls (Congcong Wang) za Dar es Salaam wameshika nafasi mbili za kwanza za kumi bora kitaifa, ambayo ina mwanafunzi mmoja kutoka shule zinazomilikiwa na Serikali.
Necta ilisema jana kuwa imetumia mfumo huo wa divisheni kutunuku matokeo ya mtihani wa kidato cha nne badala ya mfumo uliokuwa umeanzishwa wa kupanga kwa kutumia wastani wa alama (Grade Point Average, GPA) ambao Waziri wa Elimu, Profesa Joyce Ndalichako ameufuta.
Akitangaza matokeo hayo jana, Katibu Mtendaji wa Necta, Dk Charles Msonde alisema katika mkutano wa 109 uliofanyika Februari 10, baraza liliamua kurejesha mfumo wa madaraja ambao hutumia matokeo ya mitihani ya kidato cha pili na nne.
Alisema uamuzi huo ulizingatia maoni ya wadau wengi ambao walisema kuwa mfumo huo wa divisheni ndio unaoeleweka zaidi kuliko wa GPA ambao unatumia wastani wa alama.
Kwa mujibu wa mfumo huo, alama za masomo za ufaulu wa somo kwa kidato cha pili na nne ni 75 hadi 100, ambayo ni kundi “A”, 65-74 (B), alama 45-64 (C), alama 30-44 (D), wakati alama 0-29 ni kufanya vibaya.
“Uchakataji wa matokeo ya upimaji wa kidato cha pili na mitihani ya kidato cha nne na sita, utazingatia viwango vya alama, madaraja ya ufaulu na utaratibu wa matumizi ya alama endelevu (CA),” alisema Dk Msonde.
“Matumaini yetu ni mfumo huu kuwa na tija.
“Kufuatia umuhimu wa kuwa na utaratibu wa wazi wa matumizi ya alama endelevu (CA) za watahiniwa, Baraza limeamua kutumia uwiano baina ya alama endelevu (CA) na alama za mtihani wa mwisho (FE) wa 30:70 kwa watahiniwa wa shule kama unavyotumika sasa.”
Dk Msonde alisema wanafunzi 272,947 kati ya waliofanya mtihani wamefaulu, ikiwa ni asilimia 67.53 tofauti na matokeo ya mwaka 2014 wakati kiwango cha ufaulu kilipokuwa asilimia 68.33.
Kwa mujibu wa matokeo ya 2014, kiwango cha ufaulu kiliongezeka kwa asilimia 12.65 baada ya kutumia mfumo huo wa GPA, lakini mfumo mpya umeonyesha kushuka kwa asilimia 0.80.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Iringa (UoI), Jimson Sanga alisema kushuka huko kwa kiwango cha ufaulu kumetokana na kubadilishwa kwa mfumo wa upangaji matokeo. “Mfumo wa zamani ulikuwa unaficha uhalisia, na ungetumika mwaka huu ufaulu ungekuwa juu zaidi,” alisema.
Alipoulizwa kuhusu matokeo hayo, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Patrick Myovela alisema matokeo hayo yanaakisi hali ilivyo kwenye elimu kwa sasa. “Imefikia wakati baadhi ya wanafunzi hawana kitu kiasi cha kushindwa kuandika hata barua. Hii ni kwa sababu kiwango cha elimu huko chini kimeshuka sana,” alisema.
Kati ya waliofanya mtihani, asilimia 64.84 watahiniwa wasichana, wamefaulu wakati wavulana ni asilimia 71.09.
Kwa mujibu wa Dk Msonde, watahiniwa wa shule waliopata daraja la kwanza ni 5,973 sawa na asilimia 2.77 tu, wakati daraja la pili ni 19,791 (asilimia 9.01), daraja la tatu 27,749 (asilimia 13,56) na daraja la tatu la juu ni watahiniwa 53,513 (asilimia 25,34).
Waliopata daraja la nne ni watahiniwa 71.358 sawa na asilimia 67.91 na waliofeli ni 47,812 sawa na asilimia 32. Kuhusu ufaulu katika masomo, Dk Msonde alisema matokeo yanaonyesha kuwa somo la hisabati limekuwa na kiwango cha ufaulu cha asilimia 16.76 ambacho ni “cha chini kabisa” kwa watahiniwa wote wa shule.
Lakini kiwango cha ufaulu kwa somo la Kiswahili kimepanda hadi asilimia 77.63 kutoka 69.66, pamoja na somo la kemia ambalo ufaulu umepanda kutoka asilimia 56.73 hadi 60.11.
Jumla ya watahiniwa waliojiandikisha kufanya mtihani mwaka 2015 ni 448,382, kati yao wasichana wakiwa 229, 144 sawa na asilimia 51.1 na wavulana 219,238 sawa na asilimia 48.9.
Alisema kati ya watahiniwa waliosajiliwa watahiniwa wa shule walikuwa 394,065 na watahiniwa wa kujitegemea walikuwa 54,317.
Kati ya watahiniwa 448,382 waliosajiliwa kufanya mtihani, wapatao 433,633 sawa na asilimia 96.71 walifanya mitihani na watahiniwa 14,749 sawa na asilimia 3.29 hawakufanya, alisema Dk Msonde.
Kati ya watahiniwa 394,065 waliosajiliwa, 384,300 ambao ni asilimia 97.52 walifanya mitihani huku wasichana wakiwa 195,413 na wavulana 188,887. Asilimia 2.48 hawakufanya mitihani.
Dk Msonde alisema kati ya watahiniwa 54,317 wa kujitegemea waliosajiliwa, asilimia 90 walifanya mtihani na waliosalia hawakufanya.
Matokeo yaliyozuiliwa
Baraza pia limezuia kutoa matokeo ya watahiniwa 23 wa shule ambao walipata matatizo ya kiafya na kushindwa kufanya mtihani wa baadhi ya masomo na hivyo kupewa fursa ya kukamilisha masomo waliyokosa.
Dk Msonde alisema watahiniwa 98 wa shule ambao walipata matatizo ya kiafya na kushindwa kufanya mtihani kwa masomo yote, wamepewa fursa ya kufanya mtihani mwaka huu.
Wafutiwa matokeo
Alisema pia alisema baraza limefuta matokeo yote ya watahiniwa 87 waliobainika kufanya udanganyifu.
“Kati ya watahiniwa waliobainika kufanya udanganyifu, watahiniwa 25 ni wa kujitegemea na 52 ni wa shule na 10 ni wa mtihani wa maarifa (QT),” alisema.     

Categories: