Kituo cha Pamoja chazinduliwa mpaka wa Tanzania na Kenya
Posted by Unknown on 13:47 with No comments


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Dk Augustino Mahiga, akimwagia maji mti baada ya kupanda kwenye mpaka wa Tanzania na Kenya uliopo Holili Wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro jana katika uzinduzi majengo ya Kituo cha Pamoja Mpakani (OSBP). Wanaoshuhudia ni Waziri wa Kazi na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Kenya, Phillis Kandie (katikati) na Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, William Ole Nasha (kulia).
Arusha. Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Dk Augustine Mahiga na Waziri wa Kazi na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Kenya, Phillis Kandie, wamezindua kituo cha Pamoja Mpakani (OSBP) katika mpaka wa Holili uliopo Wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro.
Kituo hicho kilichopo upande wa Holili kwa Tanzania na Taveta kwa Kenya kimejengwa kwa ufadhili wa Trade Mark East Africa kwa gharama ya Dola12 milioni za Marekani.
Dk Mahiga alisema jana kuwa kituo hicho cha Holili kitarahisisha utendaji kazi wa taasisi za Serikali zinazofanya kazi kwenye mipaka hiyo.
Alisema Serikali ya Tanzania itaendelea kuzifanyia kazi changamoto za vikwazo visivyo vya kiushuru ili kurahisisha shughuli za biashara katika nchi za Afrika Mashariki.
“Lengo la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ni kuondoa mipaka iliyowekwa na Wakoloni mwaka 1884 huko Ujerumani, sisi ni wamoja na tunapaswa kushirikiana kukuza biashara,” alisema Dk Mahiga.
Kwa upande wake, Waziri Kandie alisema ufunguzi wa kituo cha Pamoja Mpakani unatoa fursa mpya ya kukuza biashara na sekta ya utalii.
Katibu Mkuu wa EAC, Dk Richard Sezibera alisema kituo hicho ni cha kwanza kuzinduliwa katika utaratibu wa wafanyakazi wa idara zinazohusika wa nchi mbili kufanya kazi katika jengo moja.
Categories: habari
0 comments:
Post a Comment