Watumishi waidai Serikali Sh56 bilioni
Posted by Unknown on 13:46 with No comments


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, Angela Kairuki alisema hayo alipozungumza katika kipindi cha siku 100 za Serikali ya awamu ya tano kupitia televisheni ya TBC1. Picha ya Maktaba.
Dar es Salaam. Watumishi wa umma wanaidai Serikali Sh56.2 bilioni ikiwa ni malimbikizo ya madeni.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, Angela Kairuki alisema hayo alipozungumza katika kipindi cha siku 100 za Serikali ya awamu ya tano kupitia televisheni ya TBC1.
Alisema kati ya fedha hizo Sh10.2 bilioni zimeshahakikiwa na kwamba zinasubiri mfumo wa malipo.
Kutokana na malimbikizo hayo aliwataka maofisa utumishi wa halmashauri kuacha kulimbikiza madeni mapya kwa madai kuwa mengi yanatokana na uzembe.
Waziri Kairuki alisema ofisa atakayebainika kusababisha malimbikizo mapya atachukuliwa hatua za kisheria.
Alisema Serikali haiwezi kuendelea kuwavumilia maofisa wazembe wasiotimiza wajibu wao.
Alitaka taarifa za wanaoajiriwa na kupandishwa madaraja ziandaliwe mapema ili zishughulikiwe.
Hata hivyo, alisema jitihada zinaendelea kufanywa ili kumaliza deni hilo.
Pia, aliwataka watumishi kuwatumikia wananchi kwa kufuata maadili ya utawala bora na utumishi wa umma.
Alisema uadilifu kwa watumishi wa umma ni kinga dhidi ya matumizi mabaya ya ofisi.
Alisema wizara hiyo itaendelea kuhakikisha kila mtumishi anatekeleza wajibu wake ili kuleta matokeo mazuri ya falsafa ya Rais John Magufuli ya Hapa Kazi Tu.
Kuhusu mishahara hewa, alisema Serikali inatafuta taarifa za kuwapo kwa watumishi wanaoendelea kulipwa mishahara kinyume cha sheria.
alisema kuwa tatizo hilo ni la muda mrefu ambalo linaisababishia serikali hasara kubwa.
Waziri Kairuki alisema kuna changamoto kubwa ya uwiano wa mishahara katika baadhi ya taasisi nchini, hali inayotokana na sheria zinazosababisha kutokuwapo kwa uwiano huo.
Categories: habari
0 comments:
Post a Comment