Nkurunziza aponea chupuchupu
Posted by Unknown on 10:43 with No comments
Jaribio la kumpindua lashindwa, Aondoka na kurejea tena Dar.
Taarifa zilizoifika NIPASHE jana usiku zilisema kuwa Nkurunziza alikuwa anaelekea Burundi, lakini aligeuza nia baada ya kuelezwa kuwa jeshi linalomtii lilikuwa limedhibiti hali ya mambo na kwamba Meja Jenerali Niyombare, alikuwa amekimbia.
Ofisa mmoja wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Tanzania aliliambia NIPASHE kuwa, anachojua ni kwamba viongozi wote wa EAC wamereja makwao baada ya mkutano.
“Sijamuona akirejea hapa hotelini (Serena). Ninachojua ni kwamba viongozi wote wamekwisha ondoka kureja makwao,” alisema na kuomba asitajwe kwa kuwa siyo msemaji wa Wizara. Hata hivyo, baadhi ya maofisa usalama waliozungumza na NIPASHE walisema kuwa Nkurunziza alikuwa Dar es Salaam na kwamba alikuwa na mazungumzo na mwenyeji wake, Rais Jakaya Kikwete.
Habari za kiuchunguzi kutoka Hotel ya Serena zilisema maofisa wengi waliokuwa kwenye kwenye msafara wa Rais Nkurunziza walikuwa maeneo ya hoteli hiyo kama vile kiongozi angerejea maeneo hayo.
Jeshi la Burundi limetangaza kuiangusha Serikali ya Rais Pierre Nkurunziza. Hata hivyo, Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), wamepinga mapinduzi hayo na kuwataka waliohusika kuirejesha nchi hiyo katika utawala wa kisheria.
Mapinduzi hayo yamefuatia wiki kadhaa za machafuko ya kisiasa nchini humo yaliyosababishwa na hatua ya kiongozi huyo kutangaza kugombea urais kwa muhula wa tatu, huku vyama vya upinzani vikiitisha maandamano yasiyo na ukomo katika mji mkuu, Bujumbura.
Rais Nkurunziza alipinduliwa jana akiwa jijini Dar es Salaam, Tanzania kuhudhuria mkutano wa Wakuu wa EAC kujadili hali ya usalama nchini Burundi.
Mkuu wa zamani wa Shirika la Kijasusi la Burundi, Meja Jenerali Godefroid Niyombare, ndiye aliyetangaza kumpindua Rais Nkurunziza.
Hata hivyo, kwa mujibu wa gazeti la The Guardian la Uingereza, Mshauri wa Rais Nkuruzinza, Willy Niyamitwe, alikana kutokea kwa mapinduzi hayo, akiita taarifa ya Jenerali huyo kuwa ni ya utani.
Shirika la Habari la Iran (IRIB) lilimkariri Jenerali Niyombare akitangaza taarifa hizo kupitia redio binafsi ya Isangiro jijini Bujumbura, akisema:
“Kuanzia sasa, Pierre Nkurunziza, si Rais tena wa Burundi, serikali imevunjwa, makatibu wa kudumu wa mawaziri wataendesha masuala ya nchi hadi tangazo jingine litakapotolewa.”
Tangazo la Jeja Jenerali Niyombare lilikuja baada ya Jeshi la Burundi kuzizingira ofisi za Redio ya Taifa katika Jiji la Bujumbura.
Kwa mujibu wa gazeti la The Guardian, ofisa huyo Mkuu wa zamani wa Mashushu wa nchi hiyo, alichukua hatua hiyo kutokana Rais Nkurunziza kukiuka katiba ya nchi hiyo kwa kitendo chake cha kuwania muhula wa tatu wa urais.
Alitoa tangazo hilo kwa waandishi wa habari kwenye kambi moja ya jeshi iliyoko jijini Bujumbura, wakati Rais Nkurunziza akiwa nje ya nchi.
Jenerali Niyombare ambaye ni Balozi wa zamani wa Taifa hilo nchini Kenya, alikuwa amezungukwa na baadhi ya maofisa waandamizi wa Jeshi na Polisi, akiwamo waziri wa zamani wa ulinzi. Aidha, mbali na sababu ya kukiuka Katiba ya Burundi, Jenerali Niyombare alisema alimpindua Rais Nkurunziza kutokana na kukaidi wito wa jumuiya ya kimataifa, uliomtaka aheshimu katiba na makubaliano ya mkataba wa amani wa Arusha.
Aidha, kwa mujibu wa Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), Jenerali Niyombare alisema Kamati ya Taifa ya Ukombozi ilikuwa imeundwa, inayojumuisha majenerali wengine watano wa Jeshi na Polisi.
Alisema kupitia Redio ya Taifa kuwa, kazi ya chombo hicho ni kurejesha umoja wa kitaifa na kuanzisha upya mchakato wa uchaguzi katika mazingira na hali ya amani.
Awali, taarifa kutoka Burundi zilisema kuwa Polisi walilazimika kufyatua risasi na mabomu ya kutoa machozi kwa waandamanaji waliokuwa wakielekea kwenye makao ya Rais, jijini Bujumbura.
Mwandishi wa BBC aliyoko jijini humo, Maud Jullien, alisema mamia ya waandamanaji waliandamana hadi umbali wa takribani kilomita moja kutoka kwa kasri la Rais, walipovamiwa na maofisa wa usalama. Polisi walifyatua risasi na mabomu ya kutoa machozi kwa waandamanaji hao waliokaribia makao ya rais.
Hiyo ilikuwa mara ya kwanza kwa waandamanaji kukaribia kasri la rais tangu maelfu ya watu walipoanza kuandamana kupinga hatua ya Rais Nkurunziza kuwania kuingoza nchi hiyo kwa awamu ya tatu, kinyume cha mwafaka wa amani wa Arusha.
WAKUU EAC WAPINGA
Jijini Dar es Salaam, wakuu wa EAC waliokuwa wakikutana kujadili hali ya Burundi wakati mapinduzi hayo yanatangazwa, walitoa tamko wakisema hawakubaliani na hatua hiyo na kuwataka waliofanya mapinduzi hayo wairudishe nchi hiyo katika utawala wa kisheria.
Wakuu hao waliokutana ni Rais wa Tanzania, Jakaya Kikwete, wa Tanzania ambaye pia ni Mwenyekiti wa EAC; Rais wa Uganda, Yoweri Mseveni; Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta na Rais wa Rwanda, Paul Kagame.
Wengine ni Makamu wa Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa; Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AU), Nkosazana Dlamini-Zuma; Katibu Mkuu EAC, Dk. Dk. Richard Sezibera.
Rais Kikwete alizungumza na waandishi wa habari jana jioni Ikulu na kutoa maazimio yaliyofikiwa na viongozi hao baada ya kumalizika kwa mkutano huo.
MAAZIMIO
Alisema viongozi wakuu wa EAC hawakubaliani na hali iliyotokea nchini Burundi.
Alisema kutokana na hali hiyo, wametoa maazimio matatu ambayo ni kuwataka waliofanya mapinduzi warudishe nchi katika utawala wa kisheria. Azimio lingine ni uchaguzi mkuu uliokuwa ufanyike mwezi ujao nchini Burundi, usifanyike hadi hapo hali ya amani itakaporejeshwa nchini humo. Rais Kikwete alisema hali ya amani itakapokuwa shwari Burundi, uchaguzi utakapofanyika ufuate utaratibu wa kisheria na pia uzingatie makubaliano ya mwaka 2005 yaliyofikiwa Arusha.
Aliongeza kuwa viongozi hao wakuu wa nchi watakutana tena Dar es Salaam baada ya wiki mbili ili kuangalia kama hali ya amani imerejea Burundi.
HALI ILIVYOKUWA
Wakati viongozi hao wakiendelea na mkutano, baada ya kuwapo taarifa kwamba Jeshi la Burundi limeipindua nchi hiyo, watu waliokuwapo katika viwanja vya Ikulu Dar es Salaam walianza kujikusanya katika makundi kujadiliana hali hiyo.
Ilipofika saa 10:05 jioni, Rais Kikwete alitoka nje ya ukumbi kulikokuwa kunafanyika mkutano huo na baada ya dakika tatu alirejea tena huku akiwasihi waandishi wasimuulize jambo lolote kuhusiana na mambo yaliyokuwa yakijadiliwa.
Wakati viongozi hao wakiendelea na mjadala, Rais Nkurunzinza ambaye alikuwapo Dar es Salaam hadi jioni, hakuwa ameingia katika mkutano huo hadi unamalizika.
Kabla ya kumalizika kwa mkutano huo, Rais Museveni aliondoka ukumbi saa 11:03 jioni. Mkutano huo ulianza saa 6:00 mchana na kumalizika 11:20 jioni.
ULINZI WAIMARISHWA
Ulinzi katika hoteli ya Serena alikokuwa Rais Nkurunziza ulikuwa wa ‘kutisha’ ukihusisha askari polisi wenye silaha za moto pamoja na Usalama wa Taifa uliotanda kila kona ya hoteli.
Askari walikuwa na silaha yakiwamo mabomu ya kurusha. Majira ya saa 10:00 jioni, aliwasili Mkurugenzi Mkuu wa Usalama wa Taifa, Rashid Othman, ambaye taarifa zinasema kuwa alikwenda kuzungumza na Nkurunziza.
Baada ya takribani saa moja, Rais Nkurunziza alitoka nje chini ya ulinzi mkali wa maofisa Usalama wa Taifa, akiongozwa na Othman na kupanda moja kwa moja kwenye gari aina ya Land Cruiser lililokuwa na Bendera ya Burundi ambalo pia liliandikwa Burundi kwenye kibao cha namba.
Taarifa zinaeleza kuwa Rais huyo alielekea nchini kwake kwa kile kilichoelezwa ni ‘kukwama’ kwa mapinduzi.
Waandishi wa habari walizuiwa kuzungumza naye wala kumpiga picha.
AREJEA BURUNDI
Hata hivyo, taarifa zilizopatikana baadaye jana jioni na kunukuliwa na BBC, zilieleza jana jioni kuwa, Rais Nkuruziza aliondoka na ndege ya Rais wa Burundi kurudi nchini humo.
Categories: NEWS
0 comments:
Post a Comment