Serikali yakanusha kuuza eneo Polisi Oysterbay.

Posted by Unknown on 10:47 with No comments


Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Pereira Ame Silima.
Serikali imekanusha kuuza eneo la Polisi Oysterbay, jijini Dar es Salaam,   bali imeingia ubia na mwekezaji binafsi ikiwa ni miongoni mwa mikakati ya kupunguza tatizo la nyumba kwa askari.
 
Hayo yalisemwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Pereira Ame Silima (pichani), wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Kasulu Mjini (NCCR-Mageuzi), Mosses Machali, bungeni jana.
 
Machali alitaka kujua kauli ya serikali kuhusiana na eneo hilo ambalo linadaiwa kuuzwa kupitia Mpango wa Ushirikiano wa Serikali na Sekta binafsi (PPP),  ili yajengwe maduka makubwa.
 
“Serikali ina kauli gani kuhusiana na jambo hilo wakati inasema kuwa ina mpango wa kujenga nyumba kwa polisi,” alihoji mbunge huyo.
 
Silama alisema mbia huyo atajenga nyumba za polisi 350 nchini na ameanza kufanya hivyo. 
 
Naye Mbunge wa Rombo (Chadema), Joseph Selasini, alisema katika wilaya ya Rombo nyumba za polisi zimejengwa kwa mabanzi na zina wadudu aina ya kunguni na sungusungu. 
 
Aidha, alitaka kujua kwanini serikali isihamasishe wananchi kushiriki ujenzi wa vituo vya polisi.
 
Akijibu, Silima alimpiga kijembe  Selasini kuwa ameuliza swali hilo kwa sababu amechangia Sh. milioni 5 kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya polisi.
 
“Mheshimiwa Selasini anataka aonekane tu, lakini amechangia Sh. milioni 5 kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya polisi….Usaidie kutoa majibu yako kwa wenzako ili Tanzania iwe na nyumba za polisi,” alisema.
Categories: