Ajali ya daladala: gongo la mboto-ubungo

Posted by Unknown on 11:57 with No comments



Dar es Salaam. Ajali iliyotokea jana Tabata Matumbi jijini hapa, ikihusisha daladala aina ya Toyota DCM na malori mawili aina ya Scania yenye uwezo wa kubeba mzigo wa tani 10 kila moja, imesababisha vifo vya watu wanne na majeruhi 25.
Kwa mujibu wa mashuhuda ajali hiyo ilitokea saa 11 alfajiri, baada ya daladala hilo lenye uwezo wa kubeba abiria waliokaa zaidi ya 35 lililokuwa likitokea Gongo la Mboto kwenda Ubungo, kugongana na malori mawili na kuharibika kiasi cha kung’oka sehemu yote ya juu.
Mashuhuda hao walisema daladala hilo liligongana na lori lililokuwa limesheheni mchanga, kabla ya kugongana kwa mara ya pili na lori jingine lililokuwa limebeba ng’ombe likitokea Ubungo kwenda Buguruni.
Shuhuda wa ajali hiyo, John Mgendi alisema kabla ya ajali hiyo daladala na lori la mchanga yalikuwa yameongozana yakienda mwelekeo wa Ubungo.
Alisema dereva wa lori la mchanga aliyekuwa kushoto alianza kuwasha taa za kumuomba dereva wa daladala apunguze mwendo, ili lori hilo liweze kumpita na kuhamia upande wa kulia.
Mgendi alisema daladala hilo lilionyesha dalili za kupunguza mwendo, lakini wakati lori lililopoanza kumpita na kuanza kuhamia upande wa kulia, daladala liliongeza mwendo na kuligonga lori, lakini katika hali ya kujihami daladala lilihamia barabara ya kutoka Ubungo kwenda Buguruni na huko likagongana tena na lori lililokuwa limebeba ng’ombe.
Shuhuda mwingine ambaye ni dereva wa bodaboda ambaye hakupenda kutaja jina lake, alisema lori la ng’ombe lilikuwa kwenye mwendo wa kasi kuelekea mnadani, hivyo haikuwa rahisi kuepuka ajali hiyo.
“Kuna mzee hapa ameanguka baada ya kushuhudia ajali ikitokea, amekaa chini kwa dakika zaidi ya 20 bila kuamka mwili umeishiwa nguvu, ilikuwa ni ajali mbaya sana haijatokea.
Shuhuda mwingine, Charles Joseph alisema wakati wa kuwatoa majeruhi wa daladala alifanikiwa kumukoa mtoto mdogo aliyekuwa chini ya kiti, akiwa hai na hana majeraha.
“Alikuwa hana majeraha wala kulia, bali alikuwa akishangaa tu. Sikumjua mama yake wakati huo,” alisema.
Daktari Kiongozi wa Hospitali ya rufaa ya Amana, iliyopo Wilaya ya Ilala, Stanley Binagi alisema walipokea miili ya watu wanne na majeruhi 25.
Dk Binagi alisema majeruhi sita waliwapeleka katika Hospitali ya Muhimbili kutokana na hali zao kuwa mbaya zaidi. “Kabla ya hapo, idadi ya vifo vilikuwa vitatu, lakini mmoja alifariki dunia baada ya kufikishwa hapa tu na idadi ikaongezeka kuwa wanne, majeruhi 20 kati ya 25 wako hapa wengine wamepumzika na wengine wanapatiwa matibabu ya kufungwa vidonda, wengine wanafanyiwa vipimo kwa matibabu zaidi, hiyo ndiyo taarifa tuliyonayo kwa sasa,” alisema Dk Binagi.
Katika taarifa yake Dk Binagi inaonyesha waliofariki ni wanaume wanne akiwamo dereva wa daladala huku mwili wa abiria mmoja tu ndiyo ukitambuliwa.
Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Mohammed Mpinga alisema jana usiku kuwa miongoni mwa waliofariki dunia, wawili walikuwa kwenye lori na wawili ni abiria wa daladala. Alifafanua kuwa majeruhi 21 wameruhusiwa na watano bado wapo Muhimbili akiwamo dereva wa lori.     

Categories: