Waziri Lukuvi aja na mipango mipya juu ya ardhi.

Posted by Unknown on 11:59 with No comments
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi,
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi  

Dar es Salaam. Serikali imeandaa mpango kabambe wa matumizi na usimamizi wa ardhi utakaozalisha mpango mji mpya wa nchi nzima kudhibiti wapimaji na wauzaji binafsi, kuharakisha upatikanaji wa hati za umiliki wa viwanja na kuondoa migogoro ya ardhi ndani ya miaka mitano.
Mpango huo pia utahusisha upimaji wa ardhi yote nchini kwa gharama ya zaidi ya Sh2 trilioni kwa kipindi cha miaka 10 na kuweka bei elekezi ya ardhi tofauti na inayowekwa sasa kiholela na mawakala wanaonunua ardhi kwenye halmashauri.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi alisema hayo kwenye mahojiano maalumu na gazeti la Mwananchi, akielezea kuwa huo ni mpango wa Serikali ya Awamu ya Tano kumaliza migogoro ya ardhi, ambayo inasababisha mapigano na wananchi kuporwa haki zao. “Tunataka kubadilisha mfumo wa usimamizi, upangaji, umilikaji na utunzaji wa kumbukumbu kwa njia ya makaratasi na mafaili. Tunataka tutunze kwa njia ya kielektroniki,” alisema Lukuvi.
Waziri huyo alisema wizara yake imepanga kupima ardhi yote ya Tanzania ndani ya miaka 10 na kwamba Serikali imeanza kutekeleza mpango huo utakaogharimu Sh2.7 trilioni.
Mpango mkuu
Lukuvi alisema kwa sasa wizara yake inaendelea na mchakato wa kuandaa mpango mkuu (master plan) wa miji ya Dar es Salaam, Arusha na Mwanza. Alisema mwaka ujao wa fedha itaandaa mpango huo kwa miji mingine 30.
Aliwataka wananchi kutokuwa na wasiwasi wa kubomolewa nyumba zao kwa sababu ya mipango miji, akisema Serikali inafuata sheria katika kutekeleza majukumu yake, kwa hiyo mwenye haki atatendewa haki. “Mipango miji haina lengo la kupora ardhi ya wananchi, tunachotaka ni kurahisisha utoaji wa huduma. Kama itatokea baadhi ya watu watatakiwa kuhama, lazima walipwe fidia inayoendana na thamani ya mali zao,” alisema.
Mkurugenzi Msaidizi wa Mipango Miji na Vijiji, Immaculate Senje alisema hadi kufikia Julai, mipango ya miji mingine 11 itakuwa imekamilika. Alisema ramani hizo ndizo zitakazosaidia kupangilia miji vizuri ili Serikali iweze kutoa huduma nyingine za kijamii.
Senje alitaja miji ambayo kufikia Julai itakuwa imemaliza kuandaa mipango yake kuwa ni Tanga, Dar es Salaam, Iringa, Bariadi, Singida, Arusha, Mwanza, Mtwara, Musoma, Bagamoyo, Korogwe, Sumbawanga na Lindi. Alisema wizara itahakikisha kila mji nchini unakuwa na master plan yake.
Lukuvi pia alibainisha Serikali imeanzisha mpango wa kurasimisha maeneo ya makazi ambayo hayajapimwa yanayokaliwa na watu. Alisema mpango huo umeanza maeneo ya Makongo, Kimara, Chasimba, Chatembo na Chachui jijini Dar es Salaam.
Aliongeza kuwa wizara yake imeingia makubaliano na wahisani kutoka barani Ulaya kusaidia mipango ya usimamizi wa ardhi.“Lengo kuu la kupima ardhi siyo kufanya biashara ili kupata fedha, bali ni kupangilia miji yetu. Halmashauri nyingi nchini zimegeuza ardhi kuwa chanzo cha mapato, matokeo yake wanasahau kupangilia miji yao, nitalisimamia hilo,” alisema.
Aliongeza kuwa wizara yake imeanza kupitia upya sera ya ardhi ya mwaka 1995 kwa sababu wako kwenye mchakato wa kuandaa sera mpya ya nyumba na sera mpya ya makazi ili ziendane na wakati wa sasa.
Lukuvi alisema pia wameanza mchakato wa kuanzisha mamlaka ya udhibiti wa mali zisizohamishika (Rera) ili kudhibiti biashara yake zikiwamo nyumba. “Siku hizi wizara yangu inatoa hati hata kwenye apartment zilizopo kwenye ghorofa. Si lazima kujenga nyumba ardhini ndiyo upate hati, hata ukinunua apartment kwenye ghorofa unapata hati yako,” alisema.
Wakati kampuni binafsi zinanunua viwanja, kuvipima na baadaye kuviuza kwa wananchi, Lukuvi alisema kuanzia sasa wapimaji binafsi hawataenda wizarani kwake kuomba hati za viwanja, badala yake watapeleka maombi kwenye halmashauri zao.
Hatua hiyo imefuata baada ya kampuni nyingi kununua ardhi na kuuza bila kuzingatia mipango miji katika eneo husika na kusababisha ujenzi holela wa makazi.
Alisema wizara itapokea maombi kutoka halmashauri baada ya kujiridhisha mipango miji imezingatiwa.
Alisema wapimaji binafsi watashirikiana na halmashauri kupanga maeneo ya makazi na kubainisha matumizi yake. Aliongeza kuwa lazima halmashauri itangaze eneo fulani kuwa la makazi ndiyo kampuni binafsi zinunue ardhi hiyo na kuuza kwa wananchi.
Mkurugenzi wa upimaji na ramani wa Wizara ya Ardhi, Profesa Justo Lyamuya alisema kwa sasa kuna wapimaji binafsi ambao wengi ni vishoka. “Si vibaya kuwa na wapimaji binafsi, lakini wafuate utaratibu unaotakiwa. Wakishirikiana na halmashauri zao, watasaidia kutekeleza mipango tuliyonayo kupangilia miji yetu,” alisema na kuongeza: “Utaratibu wa kupima ardhi lazima uzingatie fidia kabla ya kuingia maeneo ya wananchi. Sheria inataka uthamini ufanyike, watu walipwe kisha upimaji.”
Alisema ardhi yote itasimamiwa na kuratibiwa kwa mtandao chini ya mfumo maalum unaoitwa Integrated Land Management Information system (mfumo mmoja wa taarifa za usimamizi wa ardhi).
“Yaani ramani zitakuwa ndani ya mtandao. Hati inatolewa humu, michoro hii yote ya upimaji inakuwa humu kila kitu kinakuwa kule,” alisema Lukuvi.
Bei elekezi
Waziri huyo pia alisema wizara itaweka bei elekezi ili kudhibiti uuzaji holela wa viwanja unaowanyonya wananchi.
Alisema kabla ya mkurugenzi wa mipango miji kuidhinisha kuuzwa kwa viwanja, lazima aende kwenye mpango mji mkuu kuona kama vinaendana na ramani hiyo.
Alitoa mfano wa Halmashauri ya Lindi kuwa wananchi waliuza ardhi yao kando ya bahari kwa Sh400,000 kwa ekari.
Wakati huohuo, Lukuvi alisema halmashauri iliuza viwanja kwa thamani ya Sh32 milioni. “Watu wenye hela chafu wanazificha kwenye biashara ya ardhi. Watu wanaonunua viwanja ni wale wale nchi nzima. Hawashindwi kununua viwanja sehemu yoyote,” alisema Lukuvi.     

Categories: