Mazungumzo kati ya Magufuli na Maalim seif.

Posted by Unknown on 12:00 with No comments



Dar es Salaam. Siku 10 kabla ya kufanyika kwa uchaguzi wa marudio Zanzibar, Rais John Magufuli amekutana na kuzungumza faragha na Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad ambaye ametangaza kutoshiriki uchaguzi huo.
Mazungumzo hayo yalifanyika jana katika Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam wakati Rais Magufuli alipokwenda kumjulia hali kiongozi huyo aliye katika mapumziko baada ya kutoka Hospitali ya Hindu Mandal alikokuwa amelazwa kwa matibabu.
Hata hivyo, taarifa ya Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Gerson Msigwa haikueleza kwa kina mazungumzo baina ya viongozi hao, zaidi ya kusema Rais alimpa pole na kumuombea apone haraka ili aweze kuendelea na shughuli zake kama kawaida.
Rais Magufuli alisema: “Nilishtushwa sana na taarifa za kuugua kwako, lakini sasa nafurahi kukuona ukiwa mwenye afya nzuri ikilinganishwa na taarifa nilizozipata hapo awali, nakupa pole sana.”
Maalim Seif alilazwa Hospitali ya Hindul Mandal baada ya kuugua ghafla akiwa kwenye ndege akitokea Zanzibar kwenda Dar es Salaam na aliruhusiwa juzi saa 12.30 jioni.
Hii ni mara ya pili Rais Magufuli kukutana na makamu huyo wa kwanza wa Rais wa Zanzibar tangu kuibuka kwa mgogoro wa kisiasa uliotokana na kufutwa kwa uchaguzi wa Oktoba 25, 2015.
Ingawa taarifa hiyo haikuelezwa iwapo mgogoro huo ulikuwa miongoni mwa mambo yaliyozungumzwa, wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanasema kukutana kwa wawili hao ni zaidi ya kujuliana hali.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Bashiru Ally alisema kitendo hicho kinaashiria kwamba siasa haifungi njia za mawasiliano.
Alisema kitendo hicho ni ujumbe mzito unaopunguza joto la kisiasa miongoni mwa wanachama wa CUF na CCM.
Alisema kwa nafasi ya Maalim Seif akiwa mwanasiasa, ni ishara njema katika kipindi hiki kwani wafuasi wengi wanaweza kuishia katika uhasama.
Hata hivyo, Dk Bashiru alisema uchaguzi wa marudio wa Zanzibar utakuwa na mchango mdogo wa kupunguza mpasuko wa kisiasa Zanzibar kwa kuwa Maalim Seif ni kiungo muhimu kwa upande wa upinzani.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Diplomasia, Dk Ahmed Kiwanuka alisema Dk Magufuli amefanya ubinadamu kwani ugonjwa hauna chama wala siasa.
Mara ya kwanza viongozi hao walikutana Desemba 21, mwaka jana na kujadili mgogoro wa kisiasa unaoendelea visiwani humo huku Rais akimhakikishia Maalim Seif kuendelea kudumisha amani na utulivu.
“Rais Magufuli amewapongeza Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein, Maalim Seif na viongozi wote wanaoshiriki katika mazungumzo ya kuleta hali ya uelewano Zanzibar,” ilisema sehemu ya taarifa ya mazungumzo ya awali.
Licha ya matarajio hayo, viongozi hao walikutana jana huku mazungumzo yaliyokuwa yakiendelea yakiwa yamevunjika na kila upande kuibuka na msimamo wake.
CUF na Maalim Seif wameshikilia msimamo wa kutoshiriki uchaguzi wa marudio wakiamini ule uliofutwa ulikidhi vigezo vyote na Serikali ya Zanzibar chini ya Dk Shein na CCM ikishikilia msimamo wa kurudia uchaguzi kama ilivyoamuliwa na ZEC.
Kutokana na hali hiyo, ilitarajiwa kuwa viongozi hao pamoja na suala la ugonjwa, wangekumbushana hatima ya mazungumzo yao ya Desemba.
Katika kutafuta suluhu ya uchaguzi wa Zanzibar, Maalim Seif pia aliwahi kukutana na Rais mstaafu Jakaya Kikwete siku moja kabla ya hajamaliza ngwe yake ya urais. Walikutana kwa saa moja Novemba 4, 2015 na siku iliyofuata Rais Magufuli aliapishwa.
Taarifa fupi ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu, ilisema mazungumzo hayo yalitokana na ombi la Maalim Seif na kwamba viongozi hao walikubaliana kwamba mashauriano yaendelee kufanyika baina ya pande zote zinazohusika na hali ya kisiasa Zanzibar.     

Categories: