Rais Magufuli amalizana na Rais wa kampuni ya Total
Posted by Unknown on 07:50 with No comments
Makamu wa Rais wa Kampuni ya Total Afrika Mashariki Javier Rielo amemuhakikishia Rais wa Magufuli kuwa kampuni hiyo itaanza ujenzi wa mradi wa bomba la kusafirisha Mafuta kutoka Uganda hadi bandari ya Tanga Tanzania haraka iwezekanavyo kwa kuwa fedha za kutekeleza mradi huo zipo.
Javier Rielo ametoa ahadi hiyo tarehe 14 March 2016 alipokutana na kufanya mazungumzo na Rais Magufuli Ikulu Dar es salaam ambapo imefahamika mradi huo utahusisha ujenzi wa bomba lenye urefu wa kilometa 1,410 ambalo litasafirisha mafuta ghafi mapipa 200,000 kwa siku kutoka ziwa Albert Uganda hadi bandari ya Tanga na utarajiwa kuzalisha ajira za moja kwa moja 1,500 na ajira zisizo za moja kwa moja 20,000.
Katika Mazungumzo hayo Javier amemueleza Rais Magufuli kuwa Kampuni yake inatarajia kutumia dola za kimarekani karibu bilioni 4 ambazo tayari zimeshaandaliwa ambapo pamoja na kuukaribisha uwekezaji huo mkubwa kwa Tanzania, Rais Dkt. John Pombe Magufuli ameitaka kampuni hiyo kuharakisha mchakato wa kuanza kwa mradi, na ameshauri muda wa miaka mitatu uliopangwa kuukamilisha mradi huo upunguzwe ili manufaa yake yaanze kupatikana mapema.
Kwa upande wake Waziri wa Nishati na Madini Prof. Sospeter Muhongo, amesema Wizara yake ipo tayari kuhakikisha mradi huo unafanikiwa na itatoa ushirikiano wa kutosha kuharakisha utekelezaji wake.
Prof. Mhongo amebainisha kuwa licha ya kwamba hali ya kijiografia, hali ya hewa na bandari ya Tanga vinatoa mazingira bora ya kufanikiwa kwa mradi huo, Tanzania pia inatarajia kunufaika na bomba hilo, kwa kuwa kuna tafiti mbili za mafuta zinazoendelea katika ziwa Tanganyika na ziwa Eyasi, ambazo zikikamilika kwa mafanikio inatarajiwa bomba hilo litasaidia kusafirisha mafuta yake.
Categories: NEWS
0 comments:
Post a Comment