wabunge CCM wataka mgomo.

Posted by Unknown on 09:36 with No comments

Naibu Spika, Job Ndugai.
Kikao cha 46 cha Mkutano wa 20 wa Bunge la kumi, jana kilihairishwa na wabunge wa CCM kujifungia kutaka kujua kama kiinua mgongo chao ni Sh. milioni 160 au 238 kwa kila mbunge.
 
Taarifa zilizoifikia NIPASHE zinadai kuwa wabunge hao hawajalipwa kiinua mgongo hadi jana na hawajui kitakuwa ni kiasi gani.
 
Gazeti moja la kila siku (siyo NIPASHE) mwishoni mwa Juni, mwaka huu, liliripoti kuwa wabunge hao waliwasilisha ombi la kuongezea mafao yao kutoka Sh. milioni 160 hadi 238, ambalo lilikubaliwa na rais, lakini Hazina ilipopiga hesabu wakaona wanachostahili kulipwa Sh. milioni 160 kila mmoja.
 
Hata hivyo, Bunge jioni lilishindwa  kuendelea kutokana na wabunge wa CCM kujifungia kwenye kikao cha kujadili suala hilo huku Spika akiwa na kikao cha uongozi wa Bunge.
 
Kuhairishwa kwa kikao hicho, kulitokana na kauli ya Mbunge wa Sikonge (CCM), Said Mkumba, kutoa hoja ya kuhairishwa ili wabunge wa CCM wajadili kwa kina maslahi ya walimu kwa maana ya mishahara, posho na kiinua mgongo chao.
 
Naibu Spika aliwahoji wabunge ambao waliunga mkono na kwenda kwenye kikao cha chama na alitangaza kuahirisha kikao hadi leo kwa ajili ya kukaa kama kamati kupitisha vifungu vya muswada huo.
 
Asubuhi, wakati wa mjadala wa muswada wa Tume ya Utumishi wa Walimu 2015, Mbunge wa Nzega, Dk. Khamis Kigangwala, aliomba muongozo wa Mwenyekiti, Mussa Zungu, juu ya minongono iliyopo ambayo itapelekea ratiba ya leo kubadilika.
 
Mbunge huyo ambaye ni mjumbe wa Kamati ya Uongozi, bila kuweka bayana suala husika, alisema ni vyema likaandaliwa na wabunge ili kuifanya kamati hiyo kulijadili na kutoa uamuzi.
 
Baada ya mjadala kuhitimishwa na Mawaziri kujibu hoja mbalimbali, Dk. Kigangwala aliomba muongozo na kutaja vifungu vya kanuni vinavyoweza kuondolewa kwa hoja iliyopo kwa wakati huo ili kupatia ufumbuzi suala lolote.
 
“Kanuni inaruhusu hoja inayoendelea, nipewe fursa ya kuondoa hoja ya shughuli zilizopangwa kesho, tutatue ufumbuzi ili kesho kamati ya uongozi ikikutana liwe limeisha,” alisema.
 
Aidha, Mwenyekiti alisema anatambua hoja inayozungumziwa lakini hawezi kuruhusu ikajadiliwa kwa kuwa itapata ufumbuzi na kiti cha Spika kitatoa majibu.
 
Wakati wa kikao hicho jioni, baada ya Naibu Spika, Job Ndugai, kuruhusu shughuli kuendelea, Mbunge wa Sumve, Richard Ndassa, aliomba muongozo juu wa kutaka shughuli za Bunge kusitishwa, ili washughulikie jambo lenye maslahi kwao na wafanye kazi kwa amani na akili zikiwa zimetulia.
 
Naibu Spika, aliwataka wabunge kuwa na subira kwa kuwa Tume ya huduma za Bunge imekutana na Spika huku akiwataka watulie kwa kuwa walianza vizuri hivyo wamalize vizuri. Hata hivyo, Ndassa hakuridhishwa na kauli hiyo na kutaka kikao kiahirishwe kusubiri kauli ya Tume au Spika kuzungumzia hatma yao.
 
“Sisi wabunge wako tunajitolea, tumejitolea vya kutosha, tulivyokutana ukumbi wa Msekwa mliahidi mambo yatakuwa sawa leo, kesho (leo) Bunge linavunjwa, siku haziko na sisi, unaweza kuona ni dogo kumbe ni kubwa, tumejitolea ndani na nje kwa ajili ya serikali na chama chetu,” alisema.
 
Waziri wa Tamisemi, Hawa Ghasia, aliwataka wabunge kutulia na kumaliza kazi iliyo mbele yao kwa kutanguliza busara mbele, kwa kuwa suala hilo linafanyiwa kazi.
 
Naibu Spika aliwahoji wabunge ambao waligawanyika wanaosema kikao kiahirishwe na wengine wakitaka kusiahirishwe.
 
Ndugai baada ya kupokea ushauri wa Mbunge wa Longido, Michael Laizer, aliitaka serikali kulibeba kwa uzito unaotakiwa suala hilo vinginevyo hali itakuwa mbaya siku ya kuvunja Bunge.
 
Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashililah, alipoulizwa alisema anakwenda kwenye kikao na kumtaka Mkurugenzi msaidizi wa Bunge, Said Yakubu, kusikiliza waandishi. Akizungumza na waandishi, Yakubu, alisema masuala ya kiutawala ya wabunge yaneshughulikiwa ipasavyo na kuwataka waandishi kusubiri leo kama hali hiyo itaendelea.
 
Alipotakiwa kuweka wazi masuala ya utawala, alisema hawezi kuyataja kwa kuwa yametajwa kwenye sheria na kanuni za Bunge, hivyo yote yanashughulikiwa na kila mbunge atapata stahili yake.
Categories: