IGP Mangu apangua makamanda wa Polisi

Posted by Unknown on 13:44 with No comments
Mkuu wa Polisi nchini, Inspekta Jenerali (IGP)
Mkuu wa Polisi nchini, Inspekta Jenerali (IGP) Ernest Mangu. 

Dar es Salaam. Mkuu wa Polisi nchini, Inspekta Jenerali (IGP) Ernest Mangu amefanya mabadiliko kwa baadhi ya makamanda wa jeshi hilo wa mikoa na vikosi nchini.
Katika mabadiliko hayo, aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Leonard Paul amehamishwa kwenda kuendelea na wadhifa huo katika mkoa wa Tanga na nafasi yake kuchukuliwa na Kamishna Msaidizi Mwandamizi SACP, Ulrich Matei aliyekuwa Mkuu wa Utawala Kanda Maalumu ya Dar es Salaam.
Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Mihayo Msikhela aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, amehamishwa kwenda kuwa mkuu wa kikosi cha kuzuia dawa za kulevya.
Aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Ramadhani Mungi anakuwa Kamanda wa Polisi Kikosi cha Bandari na nafasi yake inachukuliwa na ACP Wilbrod Mtafungwa ambaye alikuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe.
Aliyekuwa ofisa mnadhimu Mkoa wa Iringa, ACP Prudenciana Protas anakuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe. Aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, ACP Philipo Kalangi amehamishiwa Makao Makuu ya Polisi na nafasi inachukuliwa na aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Shinyanga, ACP Ramadhan Ng’azi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara, ACP Camilius Wambura anakuwa Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam na nafasi yake kuchukuliwa na ACP Francis Massawe kutoka Makao Makuu ya Upelelezi Dar es Salaam.
Aliyekuwa Ofisa Mnadhimu Mkoa wa Arusha, ACP Gilles Mroto anakuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Tarime/Rorya kuchukua nafasi ya ACP Gemini Mushi aliyehamishiwa Makao Makuu ya Upelelezi Dar es Salaam.
Wengine ni pamoja na Naibu Kamishna wa Polisi (DCP), Hezron Gimbi anayetoka Upelelezi Makao Makuu Dar es Salaam kwenda kuwa Mkuu wa Utawala Kanda Maalumu Dar es Salaam na aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, SACP Costantine Massawe anakuwa Mkuu wa Oparesheni wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam.
Taarifa iliyotolewa na Msemaji wa Jeshi la Polisi, Advera Bulimba jana imeeleza kuwa mabadiliko hayo ni ya kawaida kwa mujibu wa Sheria, kanuni na taratibu za jeshi hilo.

Categories: